
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa ahadi ya kuhakikisha anatoa ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa taasisi zinazojihusisha na shughuli za ujenzi na kuendeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ahadi hiyo ameitoa baada ya kufanya mazungumzo na Wakuu wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi katika Ofisi ndogo za Wakala wa Barabara (TANROADS) jijini Dar es Salaam leo, tarehe 11 Disemba 2024.
Waziri Ulega amesema kuwa majukumu ya Wizara ya Ujenzi yanajumuisha ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara, madaraja, viwanja vya ndege, vivuko, majengo ya serikali na nyumba za viongozi, na kusisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja ndio msingi wa kufanikisha malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan na serikali kwa ujumla.
Waziri Ulega amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumuamini na kumteua kuhudumu katika nafasi hiyo muhimu.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, pamoja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali zinazohusiana na Wizara, ikiwemo TANROADS, Wakala wa Majengo (TBA), TEMESA, Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), AQRB, Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT).
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Aisha, amemkaribisha Waziri Ulega na kumuhakikishia ushirikiano wa kila upande kutoka kwa menejimenti na watumishi wa wizara hiyo pamoja na taasisi zake.







Hakuna maoni: