WENYE ULEMAVU WATAMANI RUZUKU TASAF KUENDELEA.

Published from Blogger Prime Android App
Na Mwandishi Wetu

Watu wenye ulemavu nchini wameshauri Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuendelea kutoa ruzuku kwa kundi hilo ili kuwainua kiuchumi na kijamii, huku wakisisitiza umuhimu wa uhakika wa masoko.

Ushauri huu waliutoa Desemba 2 mwaka huu, siku moja kabla ya kuadhimisha Siku ya Walemavu Duniani Desemba 3, wakitumia nafasi hiyo kueleza mafanikio waliyopata baada ya kujiunga na TASAF mwaka 2014 na kuondolewa mwaka jana.

Wanufaika hao wamesema wanashukuru Mfuko kwa kubadili maisha yao kupitia fedha za ruzuku, huku wakitoa rai kwa Mfuko kuangalia uwezekano wa kuendelea kuwasaidia, na kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kusaidia wenye ulemavu.

Wanufaika hao walisema TASAF imewawezesha kuanzisha biashara kama vile kuuza karanga, kutengeneza batiki, viungo vya chai, chakula, na sabuni, hivyo kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Amina Mrupe, mwenye ulemavu wa viungo anayeishi Mlandizi Mtongani, Pwani, alisema kuwa kabla ya kujiunga na TASAF mwaka 2014, alifanya biashara ndogo za ubuyu, bisi, na karanga. Alisema alikuwanapata ruzuku ya Sh 30,000 kila mwezi, lakini baadaye alipokea Sh 12,000, ambazo alikiri kuwa ziliendelea kumsaidia.

Amina aliongeza kuwa mbali na ruzuku ya kila mwezi, alipewa mtaji wa Sh 500,000, fedha ambazo zilimwezesha kuanzisha biashara ya batiki na karanga. Alisema kwamba licha ya kuondolewa kwenye mfuko mwaka jana ili kutoa nafasi kwa wengine, TASAF ilimsaidia kubadili maisha yake.

"Nikiwa na ruzuku, nilikuwa nafanya biashara na sasa natengeneza batiki, lakini pia naendelea kuuza karanga," alisema Amina. Alimwomba Rais Samia kusaidia wenye ulemavu kwa kutoa ruzuku zitakazowawezesha kufanya shughuli za kiuchumi na kujipatia riziki.

Nuru Ally, mkazi wa Kata ya Kigogo, Dar es Salaam, pia mwenye ulemavu wa jicho, alisema wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Walemavu Duniani, anashukuru TASAF kwa kubadili maisha yake. Alisema kuwa kupitia TASAF, ameweza kutengeneza viungo vya chai, chakula kama pilau, na sabuni ya chooni, hivyo kuendesha maisha yake na familia yake yenye watoto wanne.

Nuru aliongeza kuwa kabla ya TASAF, walemavu walionekana kama watu wanaopenda kuwa ombaomba, lakini kwa sasa kupitia ruzuku hiyo, amekuwa akifanya shughuli zinazomuingizia kipato. Alisema anaomba kama kuna uwezekano wa kurudishwa kwenye mfuko, ili apate ruzuku zaidi ya kufanikisha mipango yake.

Hata hivyo, wanufaika hao walisema changamoto kubwa ni soko la kuuza bidhaa zao. Walisema kwamba wateja wanaponunua bidhaa zao, hukaa muda mrefu bila kununua tena. Walisisitiza kuwa ikiwa watapata soko la uhakika, biashara zao zitawanufaisha zaidi.




Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.