Na Mwandishi Wetu,
Zanzibar.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa sheria halali za nchi zipo tayari kumkabili mtu yeyote, kikundi au watu wenye nia ya kupandikiza siasa za ubaguzi, ukabila na udini, na kwamba hawataachwa watambe mitaani.
Akizungumza visiwani Zanzibar, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alisema ni wakati wa mikono ya sheria kuanza kufanya kazi dhidi ya watu wenye nia ya kuchochea mgawanyiko wa kijamii kupitia siasa.
“Sheria ni msumeno. Mtu au kundi la watu wanaofikiri wanaweza kufanikisha mradi hatari wa kuwagawa wananchi kwa misingi ya udini, ukabila au ubaguzi wa aina yoyote, lazima waonjeshwe ukali wa sheria,” alisema Mbeto.
Ameonya kuwa nchi nyingi duniani zimeingia kwenye migogoro na hata vita kutokana na siasa za uchochezi zinazojikita kwenye misingi ya ukabila, udini na ubaguzi, na hivyo ni lazima Tanzania ichukue hatua mapema kuzuia hali kama hiyo.
“Kuna baadhi ya wanasiasa ambao ama kwa kufilisika kisiasa au kukosa hoja, wameanza kutumia lugha za ubaguzi. Hili halikubaliki. Sheria zipo na hazitakiwi kuacha mtu atambe mtaani,” aliongeza.
Katibu huyo wa Uenezi alisema kuwa maadui wakuu wa taifa ni ujinga, umasikini na maradhi, lakini pia akaonya kuwa kuna maadui wa usalama wa taifa na amani yetu — ambao ni udini, ukabila na ubaguzi.
Mbeto alikumbusha kuwa vyama vyote vya siasa vinatakiwa kuwa na sera na mipango ya kisiasa. “Kama chama hakina sera, basi kiache siasa. Kutumia ukabila au udini kama mtaji wa kisiasa ni kwenda kinyume na sheria,” alieleza.
Amesisitiza kuwa Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa Na. 5 ya Mwaka 1992 inakataza wazi matumizi ya siasa za ubaguzi, udini na ukabila katika uwanja wa kisiasa nchini.
“Sheria zipo, lakini kama zitakaa kimya huku siasa za ukabila na udini zikistawi, baadaye vitachukuliwa kama mambo ya kawaida. Tusikubali kufika huko,” alisema kwa msisitizo.
Aidha, Mbeto alieleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya vyama vya siasa ambavyo uongozi wake wa juu umeshikwa na watu wa dini moja, kanda moja au hata kabila moja — hali ambayo ni hatari kwa umoja wa kitaifa.
#ccm #siasa #amani #usalama #nchiyetu #ukabila #udini #ubaguzi #sheriazifanye kazi #zanzibar
Hakuna maoni: