Na Mwandishi Wetu,
Zanzibar.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa viongozi wake wana jukumu la kufanya siasa safi na kutekeleza sera kwa vitendo, kwa lengo la kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar – Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amesema CCM ndicho chama pekee barani Afrika kinachoheshimu utu wa binadamu na heshima ya kila mmoja.
Mbeto amesema kuwa upinzani utaendelea kuwa na changamoto kubwa kwa miaka mingi ijayo kutokana na uimara wa sera za CCM ambazo hazibaki kwenye makaratasi pekee, bali zinatekelezwa kwa vitendo vijijini na mijini.
“Vyama vingine vingi barani Afrika vinaandaa sera nzuri na kuandika ilani bora, lakini vikishika madaraka hushindwa kutekeleza. CCM ni tofauti, sera zake huenda sambamba na utekelezaji unaoleta maendeleo yanayoonekana,” alisema Mbeto.
Amesema maendeleo yanayoshuhudiwa kila kona ya Tanzania – iwe Bara au Visiwani – yanatokana na dhamira ya kweli ya viongozi wa CCM na serikali zake kuhakikisha huduma na maendeleo haviendi mrama.
“Siku zote viongozi wa CCM hujipanga na kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha nchi inasonga mbele. Hii ndiyo sababu ya mafanikio mengi tunayoyaona leo,” aliongeza.
Mbeto pia alikosoa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kwa kutumia lugha ya matusi, kejeli na siasa za chuki majukwaani badala ya kujadili sera na mikakati ya maendeleo.
“Wananchi wanapohudhuria mikutano ya upinzani husikiliza kwa muda, lakini huondoka wanapoona matusi na ubaguzi badala ya hoja. Wanaelewa kuwa viongozi hao hawana suluhisho kwa changamoto zao,” alisema.
Alisisitiza kuwa vyama vya upinzani kama ACT, Chadema, CHAUMA, NCCR-Mageuzi na Tadea vinanufaika na miundombinu na huduma bora zinazotolewa na serikali ya CCM, ikiwemo barabara, hospitali na vifaa tiba.
“Badala ya kuzungumzia sera na maendeleo, viongozi wa upinzani hutumia majukwaa kwa matusi na siasa za kuchochea chuki. Hiyo haileti tija kwa wananchi,” alihitimisha.
Hakuna maoni: