DAR ES SALAAM.
MKUU wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Mizengo Pinda, ametoa wito kwa watumishi wa umma kujiandaa kwa maisha ya baada ya kustaafu ili waendelee kutoa mchango wao kwa jamii.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya kumuaga Makamu Mkuu wa OUT aliyemaliza muda wake, Profesa Elifas Bisanda, na kumkaribisha rasmi Makamu Mkuu mpya, Profesa Alex Makulilo, Mhe. Pinda amesema ni kosa kwa mtumishi wa umma kujiweka pembeni na jamii baada ya kustaafu. Ameeleza kuwa yeye ni mfano hai wa kuendelea kuhudumia taifa kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo ufugaji na uongozi.
Akimzungumzia Profesa Makulilo, Mhe. Pinda amesema kuwa uteuzi wake ni sahihi kwani ni zao la OUT na anaelewa vyema mfumo wa chuo hicho. Ameeleza matumaini yake kuwa Profesa Makulilo ataleta mapinduzi makubwa katika taasisi hiyo.
Kuhusu Profesa Bisanda, Mhe. Pinda amempongeza kwa mchango mkubwa alioutoa ndani ya miaka 10 ya uongozi wake, ikiwemo kuimarisha miundombinu na kueneza chuo hicho nchi nzima. Ametoa wito kwa OUT kuendelea kumtumia Profesa Bisanda kama rasilimali ya kitaaluma hata baada ya kustaafu.
Kwa upande wake, Profesa Makulilo ameishukuru serikali kwa imani iliyomuonesha na kuahidi kuendeleza mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake. Ameeleza kuwa atajikita katika kuboresha TEHAMA ili kukifanya chuo hicho kuwa na ushindani wa kitaifa na kimataifa.
Naye Profesa Bisanda amepongeza wafanyakazi wa OUT kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake, huku akijivunia kulikuza chuo hicho kitaifa. Aidha, amemuasa Profesa Makulilo kushughulikia changamoto ya madeni ya watumishi wa chuo hicho ambayo kwa sasa yamefikia takribani shilingi bilioni 9.
#pinda #outtanzania #profesabisanda #profesamakulilo #utumishiwaumma #tehama #elimuyajuu #tanzaniaelimu #chuoikuu #habarizakisiasa
#mabadilikoelimu
Hakuna maoni: