DAR ES SALAAM.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za 32 za Kimataifa za Utalii kwa ukanda wa Afrika na Asia – tukio kubwa linalotarajiwa kuvuta macho ya dunia katika jiji la Dar es Salaam mnamo tarehe 28 Juni 2025. Hafla hii, inayojulikana kama World Travel Awards, ni ishara ya kutambua nafasi ya Tanzania kama moja ya vituo muhimu vya utalii barani Afrika.
Akizungumza na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Ephraim Mafuru, alibainisha kuwa tuzo hizi zilianzishwa mwaka 1993 kwa lengo la kutambua mchango wa wadau wa sekta ya utalii katika kukuza ubora wa huduma, ubunifu na maendeleo ya kimataifa katika nyanja mbalimbali zinazohusiana na utalii.
Ameongeza kuwa kwa sasa utalii hauhusishi tu maeneo ya hifadhi na vivutio vya asili, bali umejumuisha huduma kutoka hospitali, makampuni ya mawasiliano, taasisi za fedha, hoteli, kampuni za usafiri na hata mashirika ya mitandao ya kijamii – wote wakiwa na nafasi muhimu katika uzoefu wa mtalii.
Kwa mwaka huu, jumla ya wadau 38 na taasisi 12 za serikali kutoka Tanzania wanawania tuzo mbalimbali, ikiwa ni rekodi mpya kwa nchi kushiriki kwa kiwango hicho kikubwa. Dkt. Mafuru alisema kuwa ushindi wa tuzo tano mwaka jana ulikuwa ni matokeo ya mikakati madhubuti ya serikali ya awamu ya sita katika kuboresha miundombinu, matangazo ya kidigitali na huduma kwa watalii.
Aidha, alitoa wito kwa sekta binafsi, taasisi na wananchi kwa ujumla kujiandaa kuwapokea wageni zaidi ya 500, wakiwemo wageni 300 kutoka mataifa ya nje, watakaowasili kwa ajili ya kushuhudia na kushiriki hafla hiyo ya kihistoria.
Katika kuhakikisha hafla hiyo inafanyika kwa viwango vya kimataifa, Hoteli ya Johari Rotana imetajwa kuwa mshirika mkuu wa kikao hicho. Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Ahmed Said, ameishukuru Bodi ya Utalii kwa kuichagua Johari Rotana na ameahidi kutoa huduma bora, za kisasa na zenye viwango vya juu kwa wageni wote.
Kwa upande wa huduma za afya, Hospitali ya Shifaa imeteuliwa kuwa mwenyeji wa masuala ya afya kwa tukio hilo. Meneja Masoko wa hospitali hiyo, Bi. Victoria Tarimo, amesema kuwa wamejipanga vizuri kutoa huduma za dharura, huduma ya kwanza na huduma nyingine muhimu kwa wageni wote, kuhakikisha afya na usalama vinazingatiwa kikamilifu wakati wote wa tukio.
Kwa ujumla, uandaaji wa tukio hili umeweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa mara nyingine, na ni fursa adhimu ya kuonesha uzuri wa nchi, ukarimu wa watu wake na ubora wa huduma za utalii zinazozidi kukua na kuimarika kila mwaka.
#tanzaniashine2025
#tanzaniaunforgettable
#ttb
Hakuna maoni: