KILIMANJARO
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’, amezindua rasmi jengo jipya la ofisi ya CCM Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Juni 24, 2025, huku akisisitiza umuhimu wa chama hicho kuendelea kuwaandaa, kuwachuja, kuwateua na kuwawajibisha wanachama wake kwa kuzingatia sifa, maadili na uwezo wa kiuongozi.
Akihutubia mamia ya wanachama waliohudhuria tukio hilo, Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa CCM haitatoa nafasi kwa viongozi wasiokuwa waadilifu wala wasiokuwa tayari kujitolea kwa ajili ya wananchi. Alieleza kuwa taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, chama kinahitaji viongozi wachapakazi, waaminifu, na wenye kujiepusha na vitendo vya rushwa, akisema:
“Chama cha Mapinduzi hakiwezi kuendeshwa na watu wasiokuwa na moyo wa kujitolea au wenye tamaa ya madaraka.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ndg. Patrick Boisafi, aliwahimiza wananchi kuendelea kuwa na imani na CCM, akibainisha kuwa chama hicho kinaendelea kusimamia maendeleo kwa vitendo, jambo linaloendelea kuwavutia wananchi wengi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoa huo umepokea takribani shilingi trilioni 4.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, akisema:
“Hili ni dhihirisho la dhamira ya dhati ya serikali kuwatumikia wananchi kwa vitendo.”
Katibu wa CCM Wilaya ya Same, Ndg. Amos Kusakula, alisema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 164, mradi ulioanza mwaka 2022 na kukamilika kwa mafanikio makubwa. Alieleza kuwa jengo hilo ni matokeo ya mshikamano wa wanachama, wadau na juhudi za pamoja za chama kuimarisha miundombinu yake wilayani humo.
Hakuna maoni: