📍AAHIDI MABORESHO MAKUBWA YA MIUNDOMBINU
Na Mwandishi Wetu,
Tabora.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, tarehe 23 Juni 2025, alifanya ziara katika bustani ya wanyamapori ya Tabora maarufu kama Tabora ZOO, iliyoko katikati ya Manispaa ya Tabora, kwa lengo la kukagua hali ya usimamizi na huduma zitolewazo katika bustani hiyo.
Akiwa katika ziara hiyo, Dkt. Abbasi aliwahamasisha Watanzania—hususan wakazi wa Mkoa wa Tabora, mikoa ya jirani na Ukanda wa Magharibi—kutembelea kivutio hicho cha kipekee. Alieleza kuwa Tabora ZOO ni hazina ya kiutalii inayopaswa kuthaminiwa na kutumika kwa ajili ya kupumzika, kujifunza na kuhamasisha utalii wa ndani.
> “Hii ni hifadhi ya kipekee. Kuwa na eneo la zaidi ya hekta 27 katikati ya mji ni jambo kubwa. Niwaombe wakazi wa Tabora, hii ni johari yenu. Ni bustani iliyowekwa kwa ajili yenu—mje kupumzika, kujifunza. Lakini si kwa wakazi wa Tabora tu; pia wanafunzi na watu kutoka Ukanda huu wote wanakaribishwa sana,” alisema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi alieleza kuridhishwa kwake na mandhari ya bustani hiyo na akaahidi kuwa Serikali itaendelea kufanya maboresho makubwa ya miundombinu, ikiwemo:
Ujenzi wa maeneo ya kupumzikia
Burudani kwa watoto
Huduma za chakula na vinywaji
Kuongeza idadi ya wanyamapori
Uboreshaji wa mabwawa ya maji
Aidha, Katibu Mkuu huyo alipongeza juhudi za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kuboresha huduma ndani ya bustani hiyo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Maelezo kwa Wageni (VIC), mabanda ya wanyama, na ongezeko la idadi ya wanyamapori kama simba, chui, duma, fisi na wengine wa aina mbalimbali.
Tabora ZOO ni miongoni mwa bustani chache za wanyamapori zilizopo katika maeneo ya mijini nchini na imekuwa kivutio mahususi kutokana na mandhari yake nzuri na mazingira tulivu, hivyo kuiweka katika nafasi ya juu kwenye ramani ya utalii wa mijini (urban wildlife tourism).
Hakuna maoni: