RC CHALAMILA: WENYEVITI WA MITAA NI NGUZO MUHIMU KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TANESCO


DAR ES SALAAM, JUNI 24,2025

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, leo Juni 24, 2025, amefungua rasmi kikao kazi maalum kilichoandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa ajili ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutoka Manispaa za Kinondoni na Ubungo, jijini Dar es Salaam.


Katika hotuba yake ya uzinduzi, RC Chalamila alisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi mingi ya TANESCO hufanyika moja kwa moja katika maeneo ya mitaa, hivyo kuwafanya wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuwa kiungo muhimu sana katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na mafanikio.


“Wenyeviti wa mitaa ndio wanaoishi karibu na wananchi na ndio wanaofahamu changamoto halisi. Kupitia kikao hiki, naamini mtakuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii kuhusu huduma za TANESCO na kusaidia kulinda miundombinu ya shirika,” alisema Mhe. Chalamila.


Aidha, alilipongeza Shirika la TANESCO kwa kuchukua hatua ya kuitisha kikao hicho, akisema kuwa ni njia nzuri ya kuwajengea uelewa viongozi hao kuhusu shughuli za shirika na kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, alieleza kuwa shirika hilo limeona ni muhimu kujenga mfumo wa mawasiliano ya karibu na wenyeviti wa mitaa ili kuimarisha ufanisi wa huduma. “Tunahitaji kujua wananchi wanasemaje kuhusu huduma zetu, lakini pia tunahitaji kuwaelewesha wenyeviti kuhusu majukumu yetu ili waweze kufikisha taarifa sahihi kwa jamii,” alibainisha Twange.


Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhimiza matumizi ya nishati safi, TANESCO ilimkabidhi RC Chalamila pamoja na baadhi ya viongozi wa mitaa majiko ya umeme yenye matumizi madogo ya nishati.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.