HOTUBA YA RAIS MWINYI YA KUFUNGA BARAZA LA WAWAKILISHI YATAJWA KUWA YA KIMAPINDUZI – CCM YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA SERIKALI YA SMZ


Na Mwandishi Wetu, 

Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyotoa kabla ya kulivunja Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), ni hotuba ya kimapinduzi inayodhihirisha mafanikio makubwa ya kisera na maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.


Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndg. Khamis Mbeto Khamis, amesema hotuba hiyo imeakisi ufanisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kuendeleza sekta mbalimbali, ikiwemo sekta za umma na binafsi, na imetoa picha kamili ya mafanikio halisi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025.


Mbeto amesema kuwa katika kipindi hicho, SMZ imeweka mkazo mkubwa kwenye kukuza sekta za utalii, viwanda, kilimo na michezo, pamoja na kuendeleza kwa kasi Uchumi wa Buluu, pato la mtu binafsi na mapato ya Taifa kwa ujumla.


“Katika miaka mitano iliyopita, Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutekeleza malengo ya kisera katika sekta za elimu, uwekezaji, afya, maji, uvuvi, biashara, ajira, na usafiri wa anga, pamoja na kugawa vitalu kwa kampuni za uchimbaji wa gesi na mafuta,” alisema Mbeto.


Aidha, aliongeza kuwa hotuba hiyo imeweka bayana mikakati mipya na malengo mahsusi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, kuanzia mwaka 2025 hadi 2030, ambayo inalenga kuimarisha zaidi maendeleo ya Zanzibar.


“Hotuba ya Rais Dk. Mwinyi imewafumbua macho na masikio wale wanasiasa wenye hulka ya kupotosha na kubeza juhudi za Serikali. Kila mtu msikivu amesikia na kutambua mambo yaliyofanikishwa,” alieleza Mbeto.


Mbeto alisisitiza kuwa CCM imeridhishwa kwa kiasi kikubwa na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dk. Mwinyi, na kuwa na imani kubwa na viongozi na watendaji wa Serikali hiyo.


Aidha, alisema kuwa CCM imeridhishwa na hatua madhubuti zilizochukuliwa na SMZ katika kuimarisha Umoja wa Kitaifa, kupinga ubaguzi wa aina yoyote na kusisitiza dhamira ya kuwaunganisha wananchi.


Akizungumzia baadhi ya wanasiasa wanaobeza juhudi hizo, Mbeto alisema ni aibu kubwa kwao kuendelea kupotosha ukweli ilhali mafanikio ya SMZ yako wazi na yanayogusika.


“Yote yaliyoahidiwa na Rais Dk. Mwinyi wakati wa kampeni za mwaka 2020 yametekelezwa. CCM imeendelea kuthibitisha kuwa ni chama cha ahadi na utekelezaji kwa vitendo kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025,” alisisitiza.


Kwa kuhitimisha, Katibu huyo Mwenezi alisema kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa kisera yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, CCM ina uhakika wa kushinda tena uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu huko Zanzibar.


#raisMwinyi #barazalawawakilishi #zanzibar #uchaguzi2025 #siasaTanzania #ccmzanzibar #uchumiwabuluu #serikaliyamapinduzi #mwinyitena #utekelezajiilani


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.