TANZANIA YAENDELEA KUNG’ARA KIMATAIFA: PROF. SILAYO AONGOZA KIKAO CHA VIONGOZI WA KAMISHENI YA MISITU AFRIKA



Na Mwandishi Wetu, Accra

Juni 24, 2025


Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, ameongoza kikao cha Baraza la Uongozi cha Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Barani Afrika (African Forestry and Wildlife Commission – AFWC), kinachofanyika kwa siku tatu jijini Accra, Ghana.


Kikao hicho kimewakutanisha viongozi waandamizi kutoka nchi wanachama wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kwa lengo la kujadili maendeleo, changamoto, na mikakati ya pamoja ya kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu na wanyamapori barani Afrika. Aidha, kikao hicho kinatumika kama maandalizi ya Mkutano wa 25 wa Kamisheni hiyo unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, sambamba na Maadhimisho ya Wiki ya Misitu na Wanyamapori Afrika.


Akizungumza wakati wa ufunguzi, Profesa Silayo – ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Misitu (COFO) – alisema kuwa AFWC ni jukwaa muhimu kwa nchi za Afrika kujadili sera, mafanikio, na changamoto katika sekta ya misitu na wanyamapori.


Alieleza kuwa Kamisheni hiyo pia ina jukumu la kutoa ushauri kwa FAO na nchi wanachama kuhusu sera, mipango, na mbinu bora za usimamizi wa rasilimali, kwa kuzingatia mahitaji ya kikanda.


Profesa Silayo alibainisha kuwa AFWC huchochea ushirikiano wa kikanda katika uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu na wanyamapori, na hufuatilia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kama vile:


Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC)


Mkataba wa Bioanuwai (CBD)


Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa kwa njia ya Misitu (REDD+)



Vilevile, Kamisheni hiyo huhakikisha msimamo wa pamoja wa Afrika unawasilishwa kwenye maamuzi ya Kamati ya Kimataifa ya Misitu (COFO).


Akifafanua zaidi, Profesa Silayo alisema kikao hicho ni fursa adhimu kwa Afrika kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo. Alisisitiza kuwa katika wakati huu wa changamoto za kimazingira, ongezeko la watu, na shinikizo kubwa kwa rasilimali asilia, bara la Afrika linapaswa kuwa na msimamo mmoja na hatua madhubuti za pamoja.


Miongoni mwa viongozi walioungana na Profesa Silayo katika kikao hicho ni:


Abbey Haile Gabriel, Mkurugenzi Msaidizi wa FAO – Kanda ya Afrika


Pierre Taty, Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Misitu (COFO)


Profesa Labode Popoola, Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Misitu Afrika (AFF)


Edward Kilawe, Katibu wa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika



Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC) ni chombo cha kikanda kilichoanzishwa na FAO kwa lengo la kuratibu, kushauri na kuendeleza usimamizi endelevu wa misitu na wanyamapori barani Afrika. Makao makuu ya Kamisheni yako katika Ofisi za FAO Kanda ya Afrika, Accra – Ghana.


Kwa sasa, Kamisheni hiyo inaongozwa na Tanzania kupitia Profesa Silayo, jambo linaloonyesha wazi mchango mkubwa wa taifa hilo katika majukwaa ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.