MAMLAKA YA HALI YA HEWA DUNIANI KUENDELEA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA TANZANIA KUKABILIANA NA MAAFA

 


Na Mwandishi wetu,

Geneva-uswizi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani (WMO), Bi. Celeste Saulo, ameahidi kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika kuendeleza mifumo ya tahadhari ya mapema kwa ajili ya kukabiliana na maafa kwa wakati.


Ametoa kauli hiyo tarehe 5 Juni 2025 mjini Geneva, Uswizi, wakati wa kikao cha pembezoni mwa Jukwaa la Nane la Dunia la Kupunguza Madhara ya Maafa, ambacho kilimshirikisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, pamoja na ujumbe wake.


Bi. Saulo alieleza kuwa WMO iko tayari kusaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya kitaalamu kwa watendaji wake, matumizi ya vifaa vya kisasa vya utabiri wa hali ya hewa, na kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa wakati ili kuokoa maisha na kupunguza madhara.


“Tunaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kuwa tuna historia ndefu ya ushirikiano. Tutaendelea kushirikiana katika kujenga uwezo wa ndani, kuandaa miradi ya pamoja, na kuboresha mifumo ya tahadhari za mapema yenye manufaa kwa jamii,” alisema Bi. Saulo.


Aidha, alisifu hatua mbalimbali ambazo Tanzania imechukua katika kusimamia maafa, ikiwemo kuratibu mifumo ya ufuatiliaji na utoaji taarifa mapema, hatua ambazo zimeifanya nchi kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika.


Akifafanua zaidi, Bi. Saulo alibainisha kuwa mifumo ya tahadhari ya mapema ni nyenzo muhimu katika kupunguza madhara ya majanga, kwa kuwa huwezesha upatikanaji wa taarifa za awali zinazosaidia jamii kujipanga na kuchukua hatua stahiki kabla ya janga kutokea.


Kwa upande wake, Dkt. Jim Yonazi alieleza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na WMO kwa lengo la kujenga jamii stahimilivu dhidi ya majanga mbalimbali ya asili.


Alisema kuwa Tanzania inatekeleza kwa umakini mkubwa sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa maafa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ambacho kimesaidia kurahisisha utendaji kazi wa haraka na kuratibu hatua za kukabiliana na maafa.


Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya maendeleo jumuishi na kuendeleza juhudi za pamoja kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuinufaisha jamii nzima na kuifanya dunia kuwa salama zaidi kwa wote.



#tanzania #wmo #haliyahewa #maafa #tahadhariyamapema #geneva2025 #dktjimyonazi #celestesaulo #usalama #utabiri #kujikinga


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.