MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AWATAKA WADAU KUENDELEZA JUHUDI ZA UHIFADHI WA MAZINGIRA





DODOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa wadau wote wa mazingira kuendeleza juhudi zote zilizofanyika katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, ikiwemo upandaji miti na uanzishaji wa bustani za kijani.


Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma, Dkt. Mpango amewahimiza wadau kuhamasisha matumizi ya teknolojia za urejelezaji taka ozo na plastiki, kupunguza ukataji miti holela kwa ajili ya kuni na mkaa, na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Aidha, Makamu wa Rais amesema kuwa Serikali imeweka dhamira ya kupunguza athari za uharibifu wa mazingira kwa kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia badala ya kuni na mkaa. Amesema kuwa Serikali ilitoa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya mia moja kwa siku, na kuzitaka taasisi hizo kutumia nishati safi. Kufikia Machi 2025, jumla ya taasisi 762 zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia, ambapo taasisi za umma ni 495 na za binafsi ni 267.


Makamu wa Rais pia amesisitiza kuwa jukumu la kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira linahitaji ushirikiano wa wadau wote katika ngazi zote. Amevitaka vyombo vya habari, taasisi za serikali, binafsi na asasi za kiraia kushirikiana katika utoaji wa elimu kwa umma ili kupunguza uharibifu wa mazingira nchini.


Dkt. Mpango amesema takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa hali ya mazingira nchini inazidi kuzorota, ambapo takriban asilimia 61 ya ardhi iko hatarini kuharibika. Ametaja sababu kuu kuwa ni pamoja na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu, idadi kubwa ya mifugo isiyolingana na uwezo wa malisho, ukataji wa misitu, kilimo cha kuhamahama, uchimbaji holela wa madini na upanuzi wa makazi usiozingatia mipango miji.


Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kisera na kimkakati, zikiwemo kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022–2032), pamoja na kuongeza kasi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa mfumo wa kimila.


Hatua nyingine ni pamoja na kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi kwa kushirikisha kilimo mseto, kilimo cha matuta, kilimo hifadhi, na matumizi ya mbinu za asili za hifadhi ya malisho. Serikali itaendelea kutekeleza hatua hizi kwa lengo la kuimarisha utunzaji wa mazingira nchini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.