MBETO ASEMA KUMZUIA RAIA ASIPIGE KURA NI KOSA LA JINAI

 


Na Mwandishi Wetu, 

Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kuwa uamuzi wa raia kutopiga kura kwa hiari si kosa la jinai, lakini mtu, chama au kikundi chochote kitakachowazuia wananchi kupiga kura kitakuwa kinatenda kosa la jinai.


Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema kuwa haki ya kupiga kura ni ya kila Mtanzania aliyekidhi masharti ya kisheria, na kwamba kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977, Ibara ya 74, pamoja na Sheria ya Uchaguzi Na. 2 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2024, ni kosa kumzuia mtu kupiga kura.


Mbeto alifafanua kuwa kupiga kura ni haki ya kiraia na mtu anayo hiari ya kutoshiriki, lakini yeyote atakayemzuia raia aliyejiandikisha kupiga kura atakuwa ametenda kosa la jinai.

"Kupiga kura ni haki ya kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutopiga kura ni hiari ya mtu, lakini mtu au watu wakimzuia raia asipige kura, hilo litakuwa ni kosa la jinai," alisema Mbeto.


Aidha, aliongeza kuwa kuunda genge au kundi lolote linalolenga kuzuia watu kupiga kura ni kuvunja sheria na ni kosa la jinai, japokuwa mtu mmoja mmoja asiyetaka kupiga kura hatashtakiwa.


Mbeto aliwahimiza wananchi waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

"Hayupo, na wala hatatokea mtu mwenye jeuri au ubavu wa kuzuia uchaguzi usifanyike. Uchaguzi wa nchi umetajwa na sheria na Katiba ya nchi," alisisitiza Katibu huyo.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.