Mwandishi Wetu,
Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu, kuacha mara moja kumkashifu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alilitumikia Taifa kwa miaka 23 kwa uzalendo na uaminifu.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ameeleza kuwa si jambo la busara wala la kiungwana kwa Jussa kumwita Mwalimu Nyerere "kiongozi mshenzi", huku akiwa ni miongoni mwa waasisi wa taifa hili na mwenye heshima kubwa duniani kote.
Mbeto amesema kuwa si vyema Jussa kujaribu kulinganisha upeo wake wa kisiasa na Mwalimu Nyerere, kwani hata Hayati Maalim Seif Sharif Hamad — ambaye alikuwa mpinzani wa kweli na mwaminifu — hakuwahi kumtolea kashfa Mwalimu.
"Hivi Jussa kama ni hodari wa matusi, kwanini asimuanze Maalim Seif ambaye naye ametangulia mbele ya haki?" alihoji Mbeto, akiongeza kuwa siasa safi hazijengwi kwa matusi wala kejeli.
Akizungumza kuhusu kauli za Jussa alizodaiwa kuzitoa akiwa katika kikao cha ndani cha ACT-Wazalendo Wilaya ya Kaskazini 'A', Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mbeto alisema Jussa si tu alimkejeli Mwalimu Nyerere, bali pia aliwadhalilisha viongozi wote wa CCM kwa kuwaita "majahili, wezi wa kura, wasiomcha Mungu na wasio na imani za dini".
"Kauli hizi hazina nafasi katika Tanzania yenye misingi ya amani na utu. Jussa ajue kuwa Wazanzibari hawana visasi, chuki wala vonyongo," alisema Mbeto.
Aliongeza kuwa matamshi ya Jussa yanaweza kuchochea hasama, chuki na mpasuko wa kijamii, hasa pale anapotumia dini kama chombo cha kuwashambulia wenzake kisiasa.
Mbeto alisisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu si wa kisasi bali ni wa kutimiza matakwa ya Katiba, sheria na demokrasia ya kweli. Akamtaka Jussa afanye siasa safi na kuheshimu mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika kuleta uhuru, kuasisi Muungano na kudumisha Umoja wa Kitaifa.
"Mwalimu Nyerere ameacha misingi imara ya amani, mshikamano na maadili. Si haki kumvunjia heshima hiyo," alisema Mbeto.
Hakuna maoni: