Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa mataifa duniani kuchukua hatua za pamoja, kuimarisha mshikamano wa kimataifa na kuwekeza kwa uendelevu ili kulinda uchumi wa bahari, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuhifadhi bioanuwai ya baharini.
Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari (UNOC3) unaofanyika jijini Nice, Ufaransa, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza haja ya kuwa na hatua jasiri na zilizo na uratibu madhubuti ili kuhakikisha maendeleo makubwa katika kulinda na kuendeleza bahari. Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuongeza ufadhili katika kukabiliana na changamoto zinazokumba bahari, hasa kwa kuzingatia nchi za kipato cha chini na visiwa vidogo vinavyoendelea, ambavyo hukumbwa na matatizo ya bajeti na madeni yanayokwamisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan SDG 14.
Makamu wa Rais pia ametoa wito wa kutekelezwa kwa mkataba wa Bahari Kuu (BBNJ), kupinga uchimbaji usioendelevu wa madini kwenye bahari kuu, na kuanzisha vyombo vya kisheria kukabili uchafuzi wa plastiki.
Ameongeza kuwa kuna haja ya kuimarisha sera za kisayansi, kuhamasisha uhamishaji wa teknolojia, kutumia ubunifu wa kiteknolojia, pamoja na kuunganisha maarifa ya jadi na taarifa za wakati halisi kwa usimamizi bora wa rasilimali za bahari.
Dkt. Mpango amesema ushirikiano jumuishi na wa haki unahitajika, ambapo jamii za pwani zipewe nafasi ya kuwa wahusika wakuu katika kulinda mazingira ya bahari na kutafuta suluhisho za uendelevu wake.
HATUA ZA TANZANIA KATIKA UENDELEVU WA BAHARI
Makamu wa Rais ameeleza hatua kadhaa ambazo Tanzania imechukua, zikiwemo:
Kuongeza maeneo ya hifadhi ya bahari, ili kufikia lengo la kulinda asilimia 20 ya maeneo ya maji ifikapo 2030.
Kuhamasisha uhifadhi na usimamizi shirikishi unaoongozwa na jamii, ambao unahusisha ushirikishwaji wa wadau katika maamuzi.
Kutunga na kusimamia sheria dhidi ya uvuvi haramu, na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti.
Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Uchumi wa Buluu unaolenga kuimarisha miundombinu ya baharini, kuvutia wawekezaji, kuendeleza utafiti, na kulinda mazingira.
Amesisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na mataifa mengine, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na jumuiya za kiraia ili kujenga mustakabali wa bahari wenye ustahimilivu na manufaa kwa wote.
Mkutano wa UNOC3 unawakutanisha viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia na sekta binafsi kwa ajili ya kuhamasisha utekelezaji wa SDG 14, unaolenga kulinda na kutumia kwa uendelevu rasilimali za bahari na mazingira ya pwani.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni:
"Accelerating action and mobilizing all actors to conserve and sustainably use the ocean", ikihamasisha hatua za haraka na ushirikiano wa wadau wote kulinda bahari kwa maendeleo endelevu.
Hakuna maoni: