NORLAND YAJA NA FURSA ZA AJIRA KWA VIJANA, YASISITIZA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI


NA MWANDISHI WETU,

DAR ES SALAAM.

Kutokana na changamoto ya ajira inayoendelea kuwakabili vijana wengi nchini, Kampuni ya Norland, inayojihusisha na utafiti, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa tiba za afya, imejipanga kuibua fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania ili kuwawezesha kujipatia kipato halali kwa ajili ya matumizi yao binafsi na ya familia zao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Norland, Benno Mwitumba, alisema kampuni hiyo imeanzisha mpango mahsusi wa kuwawezesha vijana kupitia mfumo wa uwakala wa bidhaa zake ambazo zinahitajika kwa wingi nchini.

 “Kuna idadi kubwa ya vijana wasiokuwa na ajira za kudumu. Sisi tuko tayari kuwapatia fursa ya kufanya kazi na kujilipa kulingana na bidii zao binafsi,” alisema Mwitumba.

Alibainisha kuwa bidhaa zinazotolewa na Norland hulenga kutibu chanzo cha matatizo ya kiafya badala ya kushughulikia dalili pekee, na zimekuwa na mafanikio makubwa kwa watumiaji wa ndani na nje ya nchi.

 “Dawa, vyakula na vinywaji vingi vinavyotumiwa kwa sasa vimesheheni kemikali ambazo husababisha sumu na usugu mwilini. Bidhaa zetu husaidia kuondoa sumu hizo na kurejesha afya bila utegemezi wa dawa za muda mrefu,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa George Simbachawene, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, alieleza kuwa Serikali haiwezi kuajiri kila mhitimu wa chuo kikuu kila mwaka. Hivyo, alisisitiza umuhimu wa vijana kujielekeza katika kujiajiri kupitia sekta kama kilimo na ujasiriamali, huku akihimiza ushiriki wa sekta binafsi katika kutoa ajira.

Mwitumba alisema Norland imesikia wito huo wa serikali na sasa inatoa fursa kwa vijana wote nchini kujiunga kama mawakala wa kusambaza bidhaa zake, ambapo kipato chao kitapimwa kulingana na juhudi na ukubwa wa mzunguko wa biashara.


Kwa upande wake, Mwekezaji Mkuu wa Norland nchini, Samuel Ikongwe, alisema huu ni wakati muafaka kwa vijana kujijenga kiuchumi kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.

“Tunaunga mkono juhudi za Serikali kupunguza tatizo la ajira. Serikali inafanya kazi kubwa kwa nafasi yake, nasi kama sekta binafsi tunawajibika kusaidia pale ambapo ajira za Serikali hazitoshelezi, kwa kuwapatia vijana fursa ya kupata kipato kupitia biashara ya bidhaa zetu,” alisema Ikongwe.

Norland ni kampuni ya kimataifa yenye makao makuu nchini China, huku makao yake ya kimataifa yakiwa Marekani. Kampuni hiyo huzalisha zaidi ya aina 40 za bidhaa za afya, na hadi sasa ipo katika zaidi ya nchi 50 duniani kote.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.