DAR ES SALAAM.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameongoza uzinduzi wa Maonyesho ya Nne (4) ya Ajira kati ya Tanzania na China yaliyofanyika katika Viwanja vya Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jijini Dar es Salaam.
Maonyesho haya yamelenga kutangaza na kuwaunganisha vijana wahitimu na wenye ujuzi kutoka Tanzania na makampuni ya Kichina yanayofanya kazi nchini. Akifungua rasmi maonyesho hayo, Mhe. Kikwete amesisitiza umuhimu wa kuenzi na kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China, huku akieleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto ya ajira nchini.
Amesema maonyesho haya yanatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 2,000 kwa Watanzania, ambapo makampuni ya Kichina yanaonesha mahitaji ya aina ya ujuzi wanaouhitaji ili vijana wa Kitanzania wenye sifa stahiki waweze kuchangamkia fursa hizo.
Aidha, Mhe. Kikwete amebainisha kuwa maonyesho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata fursa za ajira zenye tija na staha, kwa kuzingatia makubaliano kati ya serikali za Tanzania na China, yenye lengo la kufanikisha maendeleo endelevu.
Katika hatua nyingine, Waziri Kikwete amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali kupitia ofisi yake itaendelea kuratibu kwa tija masuala ya ajira nchini huku ikisimamia maslahi mapana ya Watanzania kama ilivyoelekezwa na sheria, sera, miongozo ya ajira na kazi, sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hakuna maoni: