WALIOHUDUMIWA KATIKA BANDA LA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI WAPONOiGEZA UBORA WA HUDU







DAR ES SALAAM: 

Wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameendelea kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi katika viwanja vya Maturubai, Mbagala Kizuiani, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign).


Akizungumza na waandishi wa habari, Wakili wa Serikali Mkuu Grace Thadei Komba ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kufika kwa wingi katika eneo hilo kabla ya muda wa kampeni hiyo kumalizika.


“Mwitikio umekuwa mzuri, lakini bado nawahimiza wale wote wenye matatizo ya kisheria ambao hawajafika, waje mapema. Siku zimebaki chache, na timu kubwa ya wanasheria iko tayari kuwahudumia bila upendeleo,” amesema Komba.

Ameeleza kuwa kampeni hii, iliyoanzishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa tarehe 16 Juni 2025, inalenga kuwafikia wananchi wa kipato cha chini ili wapate haki zao kwa njia ya kisheria bila gharama.


Ameongeza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashiriki kikamilifu katika kampeni hii chini ya usimamizi wa Wizara ya Katiba na Sheria, na huduma hizo zitaendelea kutolewa hadi tarehe 27 Juni 2025.


Baadhi ya wananchi waliopata huduma hiyo wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni ya msaada wa kisheria inayowafikia moja kwa moja walengwa.

“Kwanza kabisa namshukuru sana Rais Samia. Mimi ni mwananchi wa kawaida, siwezi kumudu gharama za kumlipa wakili. Lakini nimefika hapa, nimepokelewa vizuri, nimesikilizwa, na naondoka nikiwa na matumaini kuwa jambo langu litashughulikiwa kwa haki,” amesema Adolf Shirima, mmoja wa wananchi waliopatiwa huduma.

Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inaendelea kuleta matumaini mapya kwa wananchi wengi, hasa wale waliokuwa hawana uwezo wa kupata huduma hizo muhimu kutokana na changamoto za kiuchumi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.