DAR ES SALAAM:
Taasisi ya Miriam Odemba Foundation (MOF) inatarajia kufanya kampeni maalum ya kuchangia damu, kutembelea wodi za wazazi, na kutoa huduma mbalimbali za afya mnamo tarehe 25 Julai 2025, katika vituo vya afya jijini Dar es Salaam na maeneo ya jirani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo, lengo kuu la kampeni ni kuwasaidia akina mama waliojifungua pamoja na wale walioko katika hali ya uzazi, ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na uzazi.
Zoezi hilo pia linakusudia kuhamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kujali afya ya wanawake, wazazi na walezi, sambamba na kuwahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika uchangiaji damu kama sehemu ya kuokoa maisha kwa njia tofauti tofauti.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mwanzilishi wa taasisi hiyo, Bi. Miriam Odemba, alisema kampeni hiyo inalenga kugusa jamii nzima na ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushiriki na kuunga mkono juhudi hizo.
> “Moyo wangu umejaa upendo na kujali vijana wa kike, ndiyo maana tunathamini watoto na wazazi wao, kwa lengo la kumjengea kijana wa Kitanzania, hususan binti wa kike, mazingira bora ya maisha,” alisema Miriam.
Taasisi hiyo pia imetoa wito kwa wadau wa afya pamoja na watu binafsi na taasisi nyinginezo kuungana nao katika kampeni hiyo kwa njia yoyote ile watakayoguswa nayo – iwe ni kushiriki moja kwa moja, kutoa huduma, misaada ya vifaa, au michango ya kifedha.
Bi. Odemba aliongeza kuwa taasisi kwa sasa inapokea michango mbalimbali inayolenga kufanikisha shughuli hizo za kijamii.
Miriam Odemba Foundation ni taasisi inayomilikiwa na Mwanamitindo nguli wa Kimataifa, Mtanzania anayeishi Hispania, Paris na Uswisi, Bi. Miriam Odemba. Taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kumwezesha binti wa Kitanzania kufikia ndoto zake kupitia misaada ya taulo za kike kwa wanafunzi, ujenzi wa vyoo mashuleni, pamoja na kusaidia watu wenye uhitaji maalum.
Hakuna maoni: