CAPTAIN HAMAD AIPONGEZA PURA


DAR ES SALAAM.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Captain Hamad Bakar Hamad, amezipongeza Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ya Tanzania Bara na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) kwa kuendeleza ushirikiano wa kisekta.


Capt. Hamad ametoa pongezi hizo Julai 07, 2025 alipotembelea banda la PURA wakati wa maonesho ya 49 ya Saba Saba yanayoendelea jijini Dar-es-Salaam.


Akitoa maelezo kwa Capt. Hamad, Mjiolojia Mwandamizi kutoka PURA, Ebeneza Mollel,amesema, tangu kusainiwa kwa hati ya ushirikiano kati ya PURA na ZPRA mwaka 2022, taasisi hizo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika masuala mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo.


Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na usimamizi wa data za petroli, ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uandaaji wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali.


Maeneo mengine ni udhibiti na usimamizi wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli na ushiriki wa wananchi katika shughuli hizo


“Nitumie fursa hii kukujulisha kuwa taasisi hizi zimeendelea kutekeleza hati ya ushirikiano na wiki iliyopita, Julai 01, 2025, menejimenti ya PURA na ZPRA zimefanya kikao cha sita kujadili taarifa ya utekelezaji wa hati hiyo kwa mwaka 2024/25,”ameeleza Ebeneza.


Kufuatia maelezo hayo, Capt. Hamad alitoa pongezi kwa namna ambavyo PURA na ZPRA zimeendelea kushirikiana na kutoa rai kwa taasisi hizo kuenzi ushirikiano huo.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.