DAR ES SALAAM.
Katibu wa Elimu, Malezi, Mazingira na Afya wa Wilaya ya Kinondoni kupitia Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Johnson Kashasha, ambaye pia alikuwa mtia nia wa kuwania tiketi ya CCM kupeperusha bendera ya ubunge katika Jimbo la Kawe, amesema amepokea kwa moyo mkunjufu maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Ndg. Kashasha amesema licha ya kutokupitishwa katika hatua ya uteuzi, anabaki kuwa mwaminifu na mtiifu kwa maamuzi ya chama, na yuko tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Kawe.
"Nipo tayari kushirikiana kwa dhati na mgombea atakayepitishwa na chama chetu ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM mwaka 2025," alisema Kashasha.
Aidha, amewasihi wote waliokuwa wakimuunga mkono katika harakati za awali, kuelekeza nguvu hizo katika kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa rasmi na chama.
"Maslahi ya Chama Cha Mapinduzi yana nafasi ya juu kuliko maslahi binafsi. Umoja wetu ndio nguzo ya ushindi wetu," amesisitiza.
Kauli ya Kashasha inaonesha utii, ukomavu wa kisiasa na mshikamano wa kweli ndani ya CCM, huku chama kikiendelea kujipanga kwa ushindi wa kihistoria katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Hakuna maoni: