MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUJADILI MCHANGO WAKE KATIKA MAENDELEO YA TAIFA JULAI 11 DODOMA




Kuelekea Kongamano la Kitaifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali – 2025


Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, limeandaa Kongamano la Kitaifa litakalofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 11 Julai 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NaCoNGO, Jasper Lazaro Makala, alisema kongamano hilo lina lengo la kutathmini na kuenzi mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya taifa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.


“Kongamano hili linaenda sambamba na kauli mbiu: Tunathamini Miaka Mitano ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa. Ni fursa ya kuangazia mafanikio, changamoto na nafasi ya mashirika haya katika kuunga mkono juhudi za serikali,” alisema Makala.


Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 2,000 kutoka ndani na nje ya nchi, huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.


Makala alieleza kuwa kabla ya kongamano hilo la kitaifa, makongamano kama hayo tayari yamefanyika katika ngazi ya wilaya na mikoa. Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa wilaya na mikoa kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha mashirika hayo yanatambuliwa na kushirikishwa katika ajenda za maendeleo.


Aidha, aliwataka wanachama wa mashirika, wadau na wananchi watakaoshindwa kufika Dodoma kufuatilia kongamano hilo kupitia mitandao ya kijamii, ambapo litakuwa likirushwa mubashara.


Kwa upande wake, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara, Bi. Vickness Mayao, alisema kongamano hilo linakuja katika kipindi muhimu ambapo mashirika hayo yameonyesha mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.


“Ni miaka mitano sasa tangu tuanze kuandaa makongamano haya, lakini mwaka huu ni wa pekee kwa sababu tunafanya tathmini ya mchango wa mashirika haya kwa ujumla wake tangu kuanzishwa kwake,” alisema Bi. Mayao.


Naye Naomi Vicent, Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Sekta Binafsi kutoka Stanbic Bank, alisema taasisi yao imekuwa mshirika mkubwa wa mashirika yasiyo ya kiserikali, ikiwemo kusaidia kupitia programu ya incubation kwa ajili ya kuendeleza taasisi changa.


“Tumeendelea kutoa usaidizi wa kitaalamu, rasilimali na ufadhili wa miradi mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha taasisi hizi zinakuwa imara na kuleta matokeo chanya kwa jamii,” alisema Naomi.


Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio, kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi kwa maendeleo endelevu ya taifa.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.