MATUMIZI YA UMEME KIGOMA YAONGEZEKA






Na Salama Kasamalu,

Kigoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Lazaro Twange amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mheshimiwa Simon Siro, tarehe 2 Julai 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo amesema ongezeko la umeme katika Mkoa wa Kigoma ni ushahidi wa mahitaji makubwa ya nishati ya umeme Mkoani humo.


Ongezeko hili linafuatia kuunganishwa kwa Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa ya umeme Disemba 2024. Matumizi ya umeme yameongezeka kutoka Megawati 17 hadi kufikia Megawati 24.


“Ongezeko hili linaonesha wazi kwamba kulikuwepo na uhitaji mkubwa wa umeme katika Mkoa wa Kigoma. Kuunganishwa kwa Mkoa huu na Gridi ya Taifa kumeleta mabadiliko chanya", alieleza Twange. 


Aidha, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa TANESCO iko tayari kushughulikia changamoto zozote za umeme zitakazojitokeza kwa wakati, ili kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana bila usumbufu.


"Niwahakikishie wakazi wa Kigoma kuwa TANESCO itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya shughuli za kilimo, biashara na matumizi ya majumbani,” alisema Bw. Twange.



Pia, katika kuunga mkono jitihada ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Bw. Twange alikabidhi majiko ya umeme kwa familia ya Mkuu wa Mkoa wa Mheshimiwa Simon Siro pamoja na familia ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye na kuwaomba watumie vifaa hivyo kama mfano kwa jamii.


Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Malagarasi (MW 49.5) pamoja na Kituo cha Kupooza Umeme cha Kidahwe. Alieleza kuwa TANESCO inaendelea kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.


“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu wa Malagarasi. Hadi sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 10 na kazi inaendelea vizuri,” aliongeza Bw. Twange.


Ziara ya Mkurugenzi Mtendaji inalenga kufuatilia na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya TANESCO katika mikoa ya Kanda ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Kigoma.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.