TANZANIA KUIMARISHA HIFADHI ZA WANYAMAPORI WANAOVUKA MIPAKA






Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutekeleza programu ya hifadhi na mifumo ikolojia inayovuka mipaka ya nchi kwenye nchi mbili au zaidi ili kuongeza nguvu katika udhibiti ujangili wa maliasili na kuimarisha ulinzi wa rasimali hizo kwa maslahi mapana ya taifa na Afrika kwa ujumla


Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliaisili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi (CP.) Benedict Wakulyamba leo 02 Julai, 2025 Jijini Dodoma akifungua kikao cha wataalam wa ndani cha kujadili uanzishaji wa hifadhi inayovuka mipaka baina ya Tanzania na Zambia ambapo amesema swala hilo litasaidia kukuza maendeleo na kiuchumi katika jamii kupitia utalii wa Wanyamapori na kufungua shoroba za wanyamapori.


“Swala la uhifadhi kwenye mfumo ikolojia inayovuka mipaka inasaidia sana katika matumizi endelevu ya maliasili ikiwemo mazao yatokanayo na misitu kama vile asali pamoja na biashara ya hewa ya kaboni na hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuziongezea kipato jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo” amesema CP. Wakulyamba


Aidha, CP.Wakulyamba amebainisha maeneo muhumi jumuishi ya ushirikiano za nchi wanachama kwenye hifadhi ikiwemo ushirikiano wa mipaka baina ya nchi husika ili kusimamia rasilimali zinazovuka mipaka yao, usimamizi wa pamoja wa Maliasili jumuishi kama mifumo ikolojia, wanyamapori, misitu na rasilimali za maji ambazo huhitaji mikakati ya pamoja ya usimamizi, ushirikiano katika uhifadhi wa bioanuwai


Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Dkt. Fortunata Msoffe amesema pamoja na mambo mengine kikao hicho kitajadili kwa pamoja kuanzishwa kwa TFCA kati ya Tanzania na Zambia sambamba na kuainisha maeneo ya kiuhifadhi yaliyopo kwenye eneo hilo, rasilimali zilizopo, fursa, pamoja na shughuli mbalimbamli zinazoweza kuchochea uhifadhi na ustawi wa jamii ili kuwezesha uanzishaji wa hifadhi hiyo. 


“Tunatambua kwamba wanyapori wanahama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na maeneo haya yanakua muhimu kwa kuwa wakati mwingine waharifu wanaweza kujificha kwenye maeneo haya, kwahiyo ni muhimu kuhakikisha tunaimarisha utendaji kazi kwa kuwa na doria za pamoja” amesema Dkt. Msoffe


Dkt. Msoffe amesema kwa mara ya kwanza Tanzania iliingia makubaliano na Msumbiji kwa lengo la kuhifadhi na kulinda mfumo ikolojia wa Selous – Niassa mwaka 2007 ambayo ni hifadhi ya pili kwa ukubwa wa hifadhi zinaovuka mipaka ikitanguliwa na KAZA katika programu ya SADC-TFCAs hatua iliyosaidia kuleta pamoja wataalamu wake kusimamia, kupanga na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ulinzi na uhifadhi katika eneo la hifadhi. Na sasa Tanzania inakusudia kuanzisha Hifadhi nyingine inayovuka mipaka ambayo inaunganisha Hifadhi za Tanzania na na Zambia.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.