📍Milango ya Uwekezaji Bado Iko Wazi
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Hatua hii inalenga kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta mbalimbali, hususan sekta ya utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa TAWA, Bw. Beatus Maganja, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.
“Tunawaambia Watanzania na wawekezaji wote kwa ujumla kuwa TAWA ni mahali sahihi kwa uwekezaji. Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa mazingira wezeshi kwa wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi yetu,” alisema Maganja.
Aliongeza kuwa TAWA inasimamia maeneo yenye rasilimali adimu, vivutio vya kipekee, na mandhari ya kuvutia ambayo yanatoa fursa kubwa ya uwekezaji endelevu kwa maslahi ya taifa na uhifadhi wa maliasili.
Baadhi ya maeneo yaliyotajwa kuwa tayari kwa uwekezaji ni:
- Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park (Arusha)
- Wami-Mbiki (Morogoro)
- Mpanga/Kipengere (Mbeya na Njombe)
- Tabora ZOO
- Ruhila ZOO
- Maeneo mengine yenye fursa mbalimbali

Aidha, aliwaalika wananchi kuonja na kununua kitoweo cha nyamapori choma kilichoandaliwa kwa umahiri.
“Kwa wale ambao hawajawahi kula nyamapori choma, nyama hiyo ipo hapa. Mishikaki pia ipo pamoja na nyama ya kupeleka nyumbani. Karibuni muonje na mjionee kuwa kweli maliasili ni za kwetu sote,” alisema Dkt. Mlay.
#uwekezaji #tawa #utalii #maliasili #fursazauwekezaji #sabasaba2025 #samia2025 #tanzania
Hakuna maoni: