MBETO: OMO SIMAMA KWA MIGUU YAKO, MUACHE MAALIM SEIF APUMZIKE PEPONI


Na Mwandishi Wetu,

Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, awaeleze Wazanzibari anataka kuwafanyia nini ambacho hakijatekelezwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, na pia aache kulitumia jina la Hayati Maalim Seif Sharif Hamad kila mara, kwani ni vyema amuache apumzike kwa amani peponi.


Akizungumza katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, alisema hakuna chama kimoja cha siasa kinachounda serikali peke yake kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, marekebisho ya kumi, bali serikali huundwa kwa ushirikiano wa vyama zaidi ya kimoja.


Mbeto alisema madai ya Othman kwamba Serikali ya Zanzibar ni ya CCM pekee ni ya kupotosha, na yanaashiria kuchanganyikiwa kwa kiongozi huyo ambaye aliwahi kuheshimika akiwa Mkurugenzi wa Mashitaka na baadaye Mwanasheria Mkuu wa SMZ.


“Serikali ya Awamu ya Nane imeundwa kwa ushirikiano wa vyama vitatu; CCM, ACT-Wazalendo na ADA-TADEA. Hivyo kudai kuwa ni serikali ya chama kimoja tu, ni zaidi ya uongo,” alisema Mbeto.


Mbeto aliongeza kuwa Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ndiye mshauri mkuu wa Rais ndani ya Baraza la Mapinduzi, na hivyo kama hakuwa akiridhishwa na maamuzi ya serikali, alipaswa kuyapinga akiwa ndani ya vikao halali, siyo hadharani.


“Mipango, mikakati na maamuzi ya SMZ hupitishwa ndani ya Baraza la Mapinduzi. OMO akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais alishiriki vikao hivyo. Angekuwa hakubaliani na sera za serikali, angepinga ndani ya kikao, siyo kujifanya mpinzani nje ya serikali,” alisema Mbeto.


Mbeto alisisitiza kuwa kitendo cha Othman kusimama hadharani na kudai kuwa SMZ ni ya CCM pekee, ni usaliti kwa chama chake ambacho ni mshirika halali wa serikali.


“Mfikishieni salamu OMO. Ajiamini, asimame kwa miguu yake mwenyewe na kujenga hoja. Kila mara akisimama anamtaja Maalim Seif – huu ni udhaifu wa kiuongozi. Dunia inamuona hawezi kujitegemea, anajificha kwenye kivuli cha Maalim Seif,” aliongeza Mbeto.


Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.