TFS YAASA JAMII KUILINDA MISITU NA KUPANDA MITI KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI



Dar es Salaam, Julai 6, 2025.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika upandaji miti na kulinda misitu ili kusaidia juhudi za serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi bioanuwai, na kukuza uchumi wa taifa.


Akizungumza kabla ya ufunguzi wa Siku ya Mazingira kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) katika Ukumbi wa Rashid Mfaume Kawawa – Ceremonial Dome, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Meneja wa Sehemu ya Baiolojia ya Mbegu za Miti TFS, Bw. Fandey Mashimba, alisema Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha upandaji miti unakuwa endelevu na wenye tija.


Kwa mujibu wa Mashimba, Tanzania inakadiriwa kuwa na hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo la ardhi ya Tanzania Bara, ambapo zaidi ya nusu ya misitu hiyo ipo chini ya usimamizi wa serikali kuu, serikali za vijiji, na mamlaka za mitaa.


“Kwa mwaka tunapoteza zaidi ya hekta 469,000 za misitu kutokana na kilimo cha kuhama hama, uvunaji haramu, na matumizi holela ya kuni na mkaa. Upandaji miti wa kimkakati ni suluhisho. Ni lazima tupande miti mingi, na yenye kulingana na ikolojia ya maeneo husika,” alisema Mashimba.


Mashimba alitoa wito kwa wananchi, sekta binafsi na washirika wa kimataifa kushirikiana na TFS katika uwekezaji kwenye miradi ya upandaji miti na kuitunza, ili kusaidia kulinda vyanzo vya maji, kuboresha ikolojia, na kupunguza upungufu wa rasilimali za misitu.


Aidha, alisisitiza matumizi ya mbegu bora za miti kutoka katika vyanzo salama, ikiwa ni pamoja na misitu ya kupandwa na misitu ya asili. Alibainisha kuwa TFS inahitaji miche milioni 440 kila mwaka ili kutimiza malengo ya kitaifa na kimataifa, yakiwemo yale ya mpango wa AFR100 ambao TFS ndiyo mratibu wa kitaifa.


Akizungumzia mchango wa misitu, Mashimba alisema kuwa mbali na kuhifadhi maji na bioanuwai, misitu hutoa ajira na kipato kupitia biashara ya mazao ya misitu, ufugaji nyuki, na utalii wa ikolojia. Aliongeza kuwa miradi ya kaboni ni fursa muhimu ya mapato na kupunguza gesi joto, lakini akasisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii kuhusu mikataba ya miradi hiyo ili izingatie miongozo ya kitaifa na kimataifa kwa manufaa ya nchi na wananchi.


Kuhusu changamoto za kampeni za upandaji miti, Mashimba alitaja baadhi kuwa ni pamoja na kufa kwa miche kutokana na uangalizi duni, ushiriki mdogo wa sekta binafsi, ukosefu wa mipango bora ya matumizi ya ardhi, na migogoro ya ardhi. Hata hivyo, alieleza kuwa TFS inaendelea kushirikiana na serikali, asasi za kiraia, na taasisi za utafiti kama Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ili kuimarisha juhudi za pamoja.


Akihitimisha, Mashimba alisema ushirikiano wa wadau wote ni muhimu ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa ya kijani kwa vizazi vijavyo.


“Misitu ni uhai wa sekta nyingine kama vile vyanzo vya maji na uchumi wa taifa. Upandaji na utunzaji wa miti ni msingi wa uhifadhi wa mazingira na unachangia kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa,” alisisitiza.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.