TUME YA MADINI YAPONGEZWA KWA KUTOA LESENI KWA WACHIMBAJI WADOGO KWA KUZINGATIA UTUNZAJI WA MAZINGIRA
Dar es Salaam, Julai 6, 2025
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja, ameipongeza Tume ya Madini kwa hatua yake ya kutoa leseni za uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo kwa kuzingatia vigezo vya utunzaji wa mazingira.
Ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake katika banda la Tume ya Madini kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam. Mhandisi Luhemeja amesema hatua hiyo ni muhimu katika kudhibiti uchimbaji holela na kupunguza uharibifu wa mazingira.
“Zamani wachimbaji wadogo walikuwa wanaingia kwa nguvu kwenye maeneo ya uchimbaji bila kufuata utaratibu wowote, mara nyingi wakichimba bila kuwa na leseni. Hali hiyo ilisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira,” amesema.
Aidha, ameitaka Tume kuhakikisha inasimamia kikamilifu utekelezaji wa masharti ya leseni hizo ili kulinda mazingira ipasavyo.
Kwa upande wake, Afisa Sheria Mwandamizi wa Tume ya Madini, Bw. Damian Kaseko, amesema Tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Madini. Majukumu hayo ni pamoja na kutoa leseni za uchimbaji, kusimamia biashara ya madini nchini, na kusuluhisha migogoro ya ardhi katika maeneo ya uchimbaji.
Bw. Kaseko ameongeza kuwa utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo hufuata taratibu madhubuti, ikiwemo uwasilishaji wa Mpango wa Utunzaji na Uendelezaji wa Mazingira (Environmental Protection Plan – EPP) kabla ya kuidhinishiwa leseni ya uchimbaji katika eneo husika.
Hakuna maoni: