MCHAKATO WA KUWAPATA WAGOMBEA KUPITIA CCM WAENDELEA, HAMASA YA MAKADA KUTIA NIA YAVUNJA REKODI - ZAIDI YA 20,000 WACHUKUA FOMU

 


DAR ES SALAAM, JULAI 03,2025.

Katibu wa Itikadi, Mafunzo na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Amosi Makala, ametoa taarifa kwa umma kuhusu mchakato wa ndani wa chama hicho katika kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge, na viti maalum kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.


Mchakato huo ulianza rasmi tarehe 28 Juni 2025 na kuhitimishwa tarehe 2 Julai 2025, ambapo wanachama na makada wa chama hicho walijitokeza kwa wingi kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi mbalimbali.


Akizungumza jijini Dodoma, Ndugu Makala aliwashukuru na kuwapongeza wanachama kwa kujitokeza kwa wingi, akisema mwamko huo mkubwa ni uthibitisho wa namna Chama Cha Mapinduzi kinavyokubalika na kuaminika katika jamii.


"Mmeona makundi mbalimbali yakichukua na kurejesha fomu; tumeona wasanii, wanahabari, maafisa, na watu kutoka nyanja mbalimbali wakijitokeza kwa wingi kuomba ridhaa ya chama chetu pendwa cha CCM," alisema Makala.


Katika taarifa hiyo, Makala alieleza kuwa jumla ya wagombea waliowasilisha fomu za ubunge na uwakilishi ni 5,475. Kati yao:

4,109 waliomba kugombea ubunge wa majimbo kutoka Tanzania Bara
524 kutoka Zanzibar
503 waliomba uwakilishi Zanzibar
623 kupitia UWT
91 kutoka makundi maalum
161 kutoka UVCCM (Zanzibar 7)
55 kutoka Jumuiya ya Wazazi
3 waliomba ubunge viti maalum Zanzibar
4 waliomba uwakilishi wa viti maalum Zanzibar
263 wanawake waliogombea ubunge majimboni
➤ Kwa upande wa udiwani, zaidi ya 15,000 wamejitokeza kugombea katika kata 3,960


MCHAKATO WA UCHUJAJI NA UTEUZI

Kuanzia kesho, vikao vya uchujaji vitaanza katika ngazi ya kata kwa ajili ya kuchambua majina ya wagombea.


Kamati za Siasa za Mikoa zitakutana tarehe 9 Julai 2025 kwa ajili ya kuwachambua wagombea wa udiwani.


Kamati Kuu ya CCM itakutana tarehe 19 Julai 2025 kwa ajili ya kufanya uteuzi wa wagombea wa ubunge.



Kwa mujibu wa Katibu huyo, mwaka huu kutakuwa na utaratibu mpya ambapo wagombea wote watafanyiwa uchambuzi na Kamati Kuu kwa kushirikiana na Kamati za Mikoa, na baadaye watateuliwa wagombea watatu kutoka kila eneo ambao watapigiwa kura za maoni.


Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kupitia Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imesisitiza kuwa mchakato wa uchujaji uwe huru na wa haki. Ametoa wito kwa vikao vyote vya uteuzi kuhakikisha haki inatendeka na ionekane ikitendeka.


“Chama cha Mapinduzi kimefurahishwa sana na hamasa iliyooneshwa na wanachama wetu kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali,” alihitimisha Makala.





Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.