TPA YAONGOZA MAKUBALIANO YA UHAMISHAJI MIZIGO KWENDA BANDARI KAVU YA KWALA – TRC, TASAC, TEAGTL WASHIRIKI
Na Mwandishi Wetu.
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi zinazohusika na huduma za bandari, imetia saini makubaliano ya taratibu za uendeshaji, uhamishaji, uhifadhi na usafirishaji wa shehena kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Bandari Kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam jana, yakihusisha wadau muhimu kama Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), na kampuni binafsi kama Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL).
Akizungumza baada ya utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, alisema kuanzishwa kwa Bandari Kavu ya Kwala kumetokana na ongezeko kubwa la shehena bandarini lililotokana na maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na wawekezaji kama DP World na TEAGTL.
“Maboresho haya yameiongezea bandari yetu mvuto kwa wateja kutoka nchi jirani, hivyo tukahitaji kuipanua kimkakati kupitia Kwala. Tayari tumeshajenga sehemu ya awali yenye hekta tano na tunaelekea kwenye awamu ya pili ya upanuzi,” alisema Mbossa.
Alibainisha kuwa kwa sasa mizigo inapelekwa Kwala kupitia reli ya zamani (MGR), na muda si mrefu reli ya kisasa (SGR) nayo itaanza kutumika rasmi kwa usafirishaji wa mizigo, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Kadogosa, aliahidi ushirikiano wa karibu kuhakikisha uhamishaji wa mizigo hadi Kwala unatekelezwa kwa mafanikio.
“Tunaunga mkono jitihada hizi kwa kuwa zinachochea maendeleo ya uchumi na kupunguza changamoto za usafiri jijini,” alisema.
Mkurugenzi wa TASAC, Mohamed Salum, alisema hatua hiyo itawanufaisha wafanyabiashara kwa kuongeza ufanisi wa kupokea bidhaa na kuongeza mapato ya serikali.
Naye Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa TEAGTL, Laksiri Nonis, aliipongeza serikali kwa hatua hiyo akisema itaimarisha ushindani wa bandari ya Dar es Salaam katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ifikapo Julai 31, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala pamoja na safari ya kwanza ya treni ya SGR ya kusafirisha mizigo ya makasha kuelekea mkoani Dodoma.
---
#bandarikavuyakwala #tpa #trc #tasac #teagtl #reliyakisasa #uchumiwataifa #raisamiasuluhu #sgrmizigo #maboresho #bandariyadasalaam #kwalamkoaPwani
Hakuna maoni: