Na Mwandishi Wetu.
Wadau wa kilimo duniani wametumia Mkutano wa Kimataifa wa Haki za Wakulima kujadili namna kifungu cha tisa cha Mkataba wa Kimataifa wa Rasilimali za Vyakula na Kilimo (ITPGRFA) kinavyoweza kusaidia kushughulikia changamoto za dharura, ikiwamo misukosuko ya kisiasa na majanga ya asili.
Mkutano huo wa pili ulifanyika hivi karibuni jijini Manila, Ufilipino, ambapo taasisi zisizo za kiserikali kutoka Tanzania ziliwakilishwa na Mtaalamu wa Sera na Utafiti kutoka Mtandao wa Baionuai (TABIO), Daud Manongi.
Akizungumzia kikao hicho, Manongi alisema hoja ya dharura kuhusu mustakabali wa wakulima ndiyo iliyotawala mijadala. Alitaja mataifa yaliyoathirika na misukosuko ya kisiasa kuwa ni Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Myanmar na Haiti.
Kwa upande mwingine, alisema changamoto za majanga ya asili zilizojadiliwa ni pamoja na vimbunga, ukame na milipuko ya visumbufu, ambazo zimekuwa zikitishia ustawi wa wakulima.
“Kwa mujibu wa mjadala huo, dharura hizo zimesababisha uharibifu wa mifumo ya mbegu na mazao, kupotea kwa maarifa ya jadi ya kilimo na wakulima kushindwa kuhifadhi, kutumia, kubadilishana au hata kuuza mbegu katika kipindi wanapozihitaji zaidi,” alisema Manongi.
Aliongeza kuwa bila kuwepo mikakati mahsusi, urejeshaji wa mifumo hiyo huchukua muda mrefu na mara nyingi hufanyika bila usawa, jambo linalosababisha wakulima wadogo kukosa haki.
Katika majadiliano hayo, ilisisitizwa umuhimu wa kuweka malengo ya moja kwa moja yanayolenga kurahisisha urejeshaji wa uzalishaji, kuimarisha benki za mbegu za kijamii pamoja na kulinda na kudumisha maarifa ya jadi ya kilimo.
Sekretarieti ya Mkataba wa ITPGRFA ilikiri kuwepo kwa mfuko wa dharura, lakini ikabainisha bado kuna haja ya kuanzisha malengo yanayoendana na mazingira halisi ya dharura, huku jamii zikishirikishwa kikamilifu ili wajisikie kuwa sehemu ya utekelezaji wa haki zao.
Manongi alihitimisha kwa kusisitiza kuwa mustakabali wa haki za wakulima nyakati za dharura unategemea mikakati thabiti na jumuishi, itakayowawezesha wakulima kuendelea kuwa walinzi wa urithi wa mbegu na maarifa ya kilimo duniani.



Hakuna maoni: