Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia Desemba 2025 hadi Februari 2026 kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mpogolo amesema Halmashauri ya Ilala imejipanga kujenga vyumba vya madarasa kwa ajili ya kupokea wanafunzi wapatao 65,000, huku sekta ya elimu ikipewa kipaumbele kikubwa katika matumizi ya fedha za maendeleo.
Ameeleza kuwa miradi ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Ilala imekamilika kwa asilimia 89, changamoto kubwa ikibaki kuwa upungufu wa vyumba vya madarasa, lakini hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa ili kutatua tatizo hilo.
“Katika utekelezaji wa Ilani, jumla ya shilingi bilioni 80 zimeelekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo kati ya shilingi bilioni 347 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Natumia fursa hii kumpongeza Rais kwa kuleta neema kubwa Ilala, ambayo inaelekea kuwa wilaya ya kisasa,” amesema Mpogolo.
Katika hatua nyingine, ameagiza viongozi wa ngazi ya kata kusimamia vikundi vya mikopo ya Serikali ya asilimia 10 inayotolewa kupitia Halmashauri, kwa kushirikiana na Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Ilala, ili kuhakikisha vikundi hivyo vinanufaika kikamilifu.
Akizungumzia migogoro ya ardhi, Mpogolo amewataka viongozi wa chama na Serikali kushirikiana kwa karibu katika kutatua changamoto hizo ili kulinda amani na maendeleo ya wananchi.
Pia amewapongeza Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala, wakiwemo Madiwani na Wabunge, kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo.
Wakati huo huo, Mpogolo amesema Wenyeviti wa Serikali za Mitaa 159 wa Wilaya ya Ilala wanatarajiwa kukabidhiwa vitambulisho vya kazi hivi karibuni, huku akiwataka wavute subira kwani taratibu zote tayari zimekamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, alimpongeza Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo, Katibu Tawala wa Wilaya Charangwa Selemani pamoja na watendaji wote wa Serikali kwa kuleta maendeleo makubwa ndani ya wilaya hiyo.Amesema Ilala ina mahusiano mazuri kati ya chama na Serikali, hali inayowezesha utekelezaji mzuri wa shughuli za maendeleo.
Naye Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurudini Sheta, aliomba Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya wapatiwe mafunzo ili kuwajengea uwezo na uelewa wa majukumu yao, na kuhakikisha kila mjumbe anafanya kazi kwa weledi.



Hakuna maoni: