DKT. HOMERA AZITAKA BODI ZA WADHAMINI KUJIEPUSHA NA UBADHIRIFU WA MALI ZA UMMA


Na Mwandishi Wetu, 

Katavi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amezitaka Bodi za Wadhamini zinazosimamia taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, michezo na taasisi nyingine zinazotoa huduma kwa jamii kujiepusha na vitendo vya ubadhirifu wa mali, migogoro isiyo ya lazima na matumizi mabaya ya rasilimali, na badala yake kusimamia mali za taasisi kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kuzingatia sheria.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi za Wadhamini na watendaji wa Serikali kutoka mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora, Mbeya, Rukwa na Songwe, ulioandaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) katika Hoteli ya Home Alone mkoani Katavi, Dkt. Homera alisisitiza kuwa wadhamini wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini, Sura ya 318.

Alionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wanaokiuka sheria, kujimilikisha mali za taasisi, kufanya ubadhirifu au kukaa madarakani kinyume na katiba za taasisi zao.

“Bado ipo changamoto ya baadhi ya bodi za wadhamini kutotimiza majukumu yao kikamilifu kwa kutumia mali za taasisi kwa maslahi binafsi, kufanya ubadhirifu wa mali na fedha, kujimilikisha mali kinyume cha utaratibu na kukaa madarakani zaidi ya muda uliobainishwa katika katiba, hali inayosababisha migogoro na uvunjifu wa amani,” amesema Dkt. Homera.

Hata hivyo, amempongeza Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, kwa hatua anazochukua kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika Bodi za Wadhamini.

“Nafahamu ipo migogoro kadhaa ya muda mrefu ambayo imefika katika wizara yangu na ngazi nyingine za kitaifa. Hata hivyo, napenda wadhamini wote mfahamu kuwa hatua stahiki za kisheria na kiutawala zitachukuliwa kwa wale wote wanaokiuka misingi ya sheria na kusababisha migogoro hii kuendelea,” amesema.

Dkt. Homera amezitaka bodi za wadhamini kuwasilisha taarifa za utendaji wao kwa RITA kupitia mfumo wa kidijitali, pamoja na kufanya marekebisho ya katiba zao ili ziendane na wakati na matarajio ya taasisi husika.

Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha kila taasisi inasimamiwa na Bodi ya Wadhamini yenye uadilifu, ujuzi na uwezo wa kuhakikisha mali na rasilimali zinatumika kwa manufaa ya wanachama.

Aidha, ametoa maelekezo kwa RITA kuharakisha marekebisho ya sheria husika, kuendelea kuboresha mfumo wa kidijitali wa eRITA, kuanzisha huduma za Mobile Clinics nchi nzima ili kusogeza huduma karibu na wadau, pamoja na kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma na wadhamini kuhusu majukumu yao ya kisheria.

Miongoni mwa maagizo mengine, Dkt. Homera ameitaka RITA kufanya tathmini ya mikutano ya wadau inayoandaa ili kubaini changamoto zinazojitokeza na kuzifanyia kazi katika mikutano ijayo. Pia ameielekeza kushirikiana na wadau wengine kuongeza elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Bodi za Wadhamini kufuata misingi ya sheria na kanuni.

Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu, Bw. Frank Kanyusi, amesema hadi Februari 10, 2026 jumla ya Bodi za Wadhamini 5,211 zimesajiliwa nchini, ambapo 2,876 ni za taasisi za kijamii, 2,161 za kidini, 19 za vyama vya siasa, 24 za michezo na 150 za kifamilia.

Amesema wadhamini wamepewa mamlaka na kuaminiwa kusimamia mali za taasisi kwa faida ya wanachama au wanufaika kulingana na madhumuni ya kuanzishwa taasisi husika kama yalivyoainishwa katika katiba.

 “Hii ina maana ukiwa mdhamini unatakiwa kuhakikisha mali za wanachama zinalindwa na kutumika kwa matumizi sahihi yaliyoainishwa katika katiba ya taasisi husika,” amesema Bw. Kanyusi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.