MBUNGE WA KIGOMA MJINI AREJEA SHULENI, ATOA WITO KWA VIJANA NA WASANII KUJIONGEZA KIELIMU


DAR ES SALAAM.

Mbunge wa Kigoma Mjini amerejea rasmi kwenye masomo baada ya kukaa nje ya mfumo wa elimu kwa miaka kadhaa, akichagua kusoma katika Shule ya Brothers Academy iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mapema leo Februari 11, 2026, amesema uamuzi wake wa kurejea shule unatokana na kutambua umuhimu wa elimu katika kufungua fursa mbalimbali za maendeleo binafsi na kijamii.

Ameeleza kuwa kushindwa kuendelea na masomo awali kulitokana na msiba wa kufiwa na wazazi wake, hali iliyomlazimu kuanza kujitafutia maisha mapema ili kujikimu.

“Baada ya kufiwa na wazazi, nilianza kazi ya kutengeneza magari, baadaye nikaenda JKT na hatimaye nikajikita kwenye muziki,” amesema.

Amefafanua kuwa mwaka 2015 alichaguliwa kuwa Diwani, mwaka 2020 akajihusisha na masuala ya redio, na baadaye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, hatua ambazo zimeongeza wajibu wake kwa wananchi.

Mbunge huyo amesema kurejea shule kutamuwezesha kuongeza maarifa na ujuzi utakaomsaidia kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi katika sekta mbalimbali za maendeleo.

“Kama umepata fursa ya kusoma, soma kijana. Unaweza kuwa na kipaji, lakini bila elimu ni vigumu kufika mbali,” amesisitiza.

Aidha, ametoa wito kwa wasanii na wananchi wote waliokosa fursa ya masomo kutokata tamaa, bali kuchangamkia programu maalum za masomo zinazotolewa na Brothers Academy, ikiwemo programu ya VIP inayowawezesha wanafunzi kusoma wakiwa popote kutokana na majukumu yao.

Amesema anaunga mkono juhudi za Rais katika kuwekeza zaidi kwenye sekta ya elimu na kuwataka vijana na watu wazima waliokwama kimasomo kutumia fursa iliyopo kurejea darasani. Pia amewapongeza wabunge wenzake kwa kuonyesha mfano wa kujiendeleza kielimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Brothers Academy, Robert Rwezaula, amesema taasisi hiyo imesajiliwa chini ya mfumo wa elimu ya watu wazima na inalenga kuwasaidia wale ambao hawakupata fursa ya kumaliza masomo yao.

Ameeleza kuwa programu zao zinamwezesha mwanafunzi kukamilisha elimu ya sekondari ndani ya miaka miwili, huku kidato cha sita kikisomwa kwa mwaka mmoja kwa lengo la kupata angalau alama tatu za ufaulu (credits).

Shule hiyo pia hutoa masomo kwa wanafunzi waliofeli kidato cha nne na sita, pamoja na darasa maalum kwa walioishia kidato cha nne. Mbali na masomo ya kawaida, wanatoa mafunzo ya kompyuta na wana kampasi mbili zilizopo Ukonga na Mbagala, pamoja na programu ya VIP inayowawezesha wanafunzi kuhudumiwa popote walipo.

Amesema lengo kuu la Brothers Academy ni kuwapatia vijana na watu wazima waliokosa fursa ya masomo nafasi ya pili ya kutimiza ndoto zao za kielimu na kitaaluma.


@brothersAcademy

#brothersacademy



Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.