Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imebainisha haja ya kufanya mapitio ya haraka ya Sera na Sheria ya Huduma za Habari nchini ili kuendana na kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia ya kidijitali.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa sheria hiyo, iliyotungwa mwaka 2016 kabla ya ukuaji wa sasa wa mitandao ya kijamii, inatoa tafsiri pana itakayowawezesha bloga na watengeneza maudhui ya mtandaoni kutambulika na kusimamiwa kisheria.
Kutokana na mazingira ya sasa, JAB inaona kuna umuhimu wa kufanya mapitio hayo ili kuyaingiza katika mfumo makundi hayo mapya yanayochipukia kwa kasi katika tasnia ya habari.
Katika wasilisho lililotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, katika mkutano wa mwaka wa utangazaji 2026 jijini Dodoma, imeelezwa kuwa mfumo rasmi wa ithibati umewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, kwa lengo la kulinda maslahi ya umma na kuimarisha maadili ya kitaaluma.
Kwa sasa, JAB inasimamia utambuzi wa wataalamu wa habari kupitia mfumo wa kidigitali wa TAI-HABARI, ambapo waandishi waliokidhi vigezo hupatiwa vitambulisho (Press Cards) vyenye uhalali wa miaka miwili. Hadi kufikia Januari 2026, takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya maombi 3,200 yameidhinishwa, huku maombi mengine yakiendelea kufanyiwa kazi.
Licha ya mafanikio hayo, Bodi imetaja kuwepo kwa changamoto ya mtazamo hasi miongoni mwa baadhi ya wadau ambao wanaiona ithibati kama chombo cha kudhibiti badala ya nyenzo ya kuimarisha ubora wa uandishi.
Aidha, uelewa mdogo wa sheria umekuwa ukisababisha baadhi ya waandishi kuwasilisha maombi yasiyokidhi vigezo vya kitaaluma, ikiwemo hitaji la kuwa na angalau Stashahada au Shahada ya Uandishi wa Habari. JAB imesisitiza kuwa mwandishi asiye na ithibati hukosa uhalali wa kisheria na anaweza kuchukuliwa hatua kali, huku ikionya kuwa hali hiyo inadhoofisha uaminifu wa habari nchini.
Wakili Kipangula amesema kwamba Bodi imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kama TCRA na taasisi za elimu ili kuhakikisha kuwa ithibati inatumika kama nyenzo ya kumlinda mwandishi katika utekelezaji wa majukumu yake, kumpatia ulinzi wa kitaaluma dhidi ya vitisho, na kuhakikisha jamii inapata habari sahihi na za kweli.

Hakuna maoni: