Watumishi kutoka Wizara ya Nishati wamepongeza kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambao umefikia asilimia 81 huku ukifungua fursa nyingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa ajira na ujuzi..
Akizungumza Februari 27, 2026, Chongoleani, Tanga, Mkuu wa Msafara, Bi.Mary Kessy amesema watumishi kutoka Idara na Vitengo mbalimbali vya Wizara wameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati wenye urefu wa kilometa 1443 kutokea Hoima nchini Uganda.
Aidha, amepongeza uongozi wa Wizara kwa kufanikisha ziara hiyo ya kutembelea na kujionea utekelezaji wa mradi iliyohusisha watumishi zaidi ya 100 kutoka sekta ya nishati.
Kwa upande wake, Msimamizi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) Mha. Mussa Msafiri, amesema kazi zinazoendelea katika eneo la mradi ni pamoja na ulazaji wa mabomba, ambapo uchomeleaji wa vipande vya bomba umekamilika kwa asilimia 100.
Ameongeza kuwa ujenzi wa vituo vya kusukuma na kupunguza msukumo wa mafuta umefikia asilimia 71.6, ujenzi wa matenki umefikia asilimia 88, huku ujenzi wa jeti ukifikia asilimia 87.
Vilevile, amesema ushiriki wa TPDC katika mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuendeleza sekta ya mafuta na gesi, pamoja na kuhakikisha rasilimali za nishati zinawanufaisha Watanzania kupitia ajira, zabuni kwa wazawa na ukuzaji wa ujuzi.



Hakuna maoni: