SERIKALI YAFUNGUA MILANGO YA AJIRA KIMATAIFA, VIJANA 4,966 WAUNGANISHWA NA FURSA NJE YA NCHI.


SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imesema inaendelea na majadiliano ya kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano wa ajira na nchi 15 zikiwemo Sweden, Denmark, Poland, Oman, Ujerumani na Kuwait huku Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Oman yanatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Kauli hiyo imetolewa Jijini jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Zuhra Yunusi, wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 500 wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi katika mataifa mbalimbali ambapo Amesema kuanzia Julai 2025 hadi Februari 2026, jumla ya Watanzania 4,966 wameunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi.

Ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na mawakala binafsi wa ajira imeendelea kuratibu huduma za ajira kwa kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri wa nje na pia imeandaa Mwongozo wa Mawakala Binafsi wa Ajira wa mwaka 2025 unaolenga kusimamia na kuratibu shughuli za mawakala hao ili kulinda haki na maslahi ya Watanzania wanaopelekwa kufanya kazi nje ya nchi.

Akizungumzia masuala ya mikataba na haki za msingi, Zuhra amesisitiza kuwa mikataba yote ya ajira imehakikiwa na Serikali ili kuhakikisha inazingatia viwango vya kimataifa, maslahi ya wafanyakazi na usalama wa watanzania wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Jane Soroga, amesema vijana hao wamepewa mafunzo maalum kabla ya kuondoka nchini ambayo yamejumuisha uwajibikaji kazini, nidhamu, utunzaji wa nyaraka, uelewa wa tamaduni za nchi wanazokwenda pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto za mazingira mapya ya kazi.

Naye Afisa Mfawidhi mkuu kutoka mfuko wa taifa wa hifadhi ya Jamii-NSSF Neila kambaya ameeleza kwamba mfuko umetoa elimu kwa vijana hao kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii na tayari wamewasajili baadhi yao ili waweze kunufaika na mafao hata wanapokuwa nje ya nchi.

Nao vijana wanaoelekea ughaibuni wamesema wako tayari kuiwakilisha Tanzania kwa weledi, uadilifu na bidii na kubainisha kuwa fursa hiyo ni mwanzo wa safari ya kutimiza ndoto zao na kusaidia familia zao pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia uzoefu na kipato watakachokipata nje ya nchi.

Aidha Vijana hao wanakwenda kufanya kazi katika kada mbalimbali ikiwemo wataalamu wa lishe, mafundi ujenzi, wataalamu wa mifugo, wataalamu wa maabara pamoja na watumishi wa majumbani.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.