MAKONDA, MWANA FA NA VIONGOZI WA TFF WAKAGUA UWANJA WA BENJAMIN MKAPA KUELEKEA AFCON 2027


Februari 09, 2026

DAR ES SALAAM. 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameongoza ziara ya ukaguzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kama sehemu ya maandalizi ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Katika ziara hiyo, Waziri Makonda aliambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, Katibu Mkuu wa wizara, Gerson Msigwa, pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Makonda amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kuhakikisha uwanja huo unakidhi viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa ajili ya kuandaa mashindano hayo ya kimataifa.

Amebainisha kuwa Tanzania ipo katika hatua muhimu ya maandalizi ya AFCON 2027, ambayo itashirikishwa na nchi tatu za Afrika Mashariki — Tanzania, Kenya na Uganda — hivyo ni muhimu miundombinu iwekwe katika kiwango kinachotakiwa.

Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema ukaguzi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa kutathmini na kuboresha miundombinu ya michezo mapema ili kuepuka changamoto za dakika za mwisho.

AFCON 2027 inatarajiwa kuwa tukio la kihistoria kwa ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo nchi washirika zinaendelea kushirikiana katika kuboresha miundombinu, mipango ya kiusalama na huduma za mapokezi kwa timu na wageni.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.