TANZANIA YAPATA HESHIMA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA CAF


DAR ES SALAAM. 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda amesema jitihada mbalimbali za Serikali ya Awamu ya Sita zimezaa matunda kwa Tanzania kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Makonda ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, ambapo amesema Februari 13, 2026 Rais wa CAF Dkt. Patrice Motsepe pamoja na ujumbe wake wanatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya mkutano mkuu wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo.

Ameeleza kuwa kufanyika kwa mkutano huo nchini ni matokeo ya mazungumzo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais huyo wa CAF, ambapo Rais Samia alimshawishi kufanya baadhi ya mikutano yake muhimu hapa nchini.

Makonda ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya Tanzania kujiweka kwenye ramani ya michezo barani Afrika na duniani, pamoja na kuonesha uwezo wa nchi kuandaa matukio makubwa ya kimataifa kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza pamoja na Kenya na Uganda.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na CAF katika kukuza maendeleo ya soka na michezo mingine ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha matukio ya michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.