MKENDA: TUZO YA TAIFA YA MWALIMU NYERERE NI KICHOCHEO CHA UBUNIFU NA UTAMADUNI WA KISWAHILI


Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu imeendelea kuwa kichocheo muhimu cha kukuza ubunifu miongoni mwa waandishi wa vitabu, kuongeza uzalishaji wa vitabu vyenye ubora wa hali ya juu na kuimarisha sekta ya uchapishaji nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vya tuzo hiyo, Prof. Mkenda amesema kuwepo kwa tuzo hizo kumeongeza idadi ya vitabu bunifu vinavyoandikwa nchini, hali ambayo imechangia vitabu vya Kitanzania kuanza kununuliwa hata katika masoko ya kimataifa.

“Bila kuwepo na kichocheo kama hiki cha tuzo, kusingekuwa na hamasa kubwa ya uandishi bunifu. Hii ingeipa kazi kubwa Taasisi ya Elimu Tanzania kupata vitabu vya kufundishia shuleni na vile vya kuongeza uelewa kwa wanafunzi,” amesema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa tuzo hiyo imebeba falsafa ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye licha ya majukumu makubwa ya kuongoza taifa, alikuwa mwandishi mahiri wa vitabu, mkalimani wa fasihi na mpenzi mkubwa wa sanaa ya uandishi.

“Tuzo hizi zinachangamsha soko la vitabu nchini. Ni lazima tuwe na vitabu vyetu, watu wasome vitabu vya ndani ili waelewe utamaduni wetu wa Kitanzania, si kusoma vya nje pekee,” amesisitiza.

Prof. Mkenda amewataka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuhakikisha tuzo hizo zinalindwa na kuendelezwa kila mwaka kwa ukubwa wake, huku zikiendelea kukua na kutambulika zaidi kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Anneth Komba, amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendesha tuzo hiyo na kuchapisha vitabu bunifu vinavyotokana na washindi wa tuzo.

Amesema kati ya fedha hizo, shilingi milioni 400 zimetumika kuchapisha nakala 100,000 za vitabu mbalimbali, ambavyo vitasambazwa katika shule nchini, ambapo kila shule itapatiwa kati ya vitabu 8 hadi 10.

Dkt. Komba amesema tuzo hiyo ina malengo sita makuu, yakiwemo kuongeza ubunifu kwa waandishi wa vitabu, kukuza utamaduni wa kusoma kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, pamoja na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.

Ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kufanikisha mpango huo, akisema ni hatua kubwa ya kuwekeza katika elimu, lugha ya Kiswahili na utamaduni wa taifa.

Katika hafla hiyo, vitabu vipya vya aina tatu vilizinduliwa kwaaili ya kuchapishwa na kugawanywa katika shule mbalimbali, ambavyo ni riwaya, ushairi na hadithi za watoto.Ambqvyo ni Ngoma ya Muwele, Garasa na Maziwa ya Kuku.

Mwenyekiti wa Tuzo hizo, Profesa Penina Mlama, amesema malengo ya tuzo ni kuwatambua na kuwajengea uwezo waandishi wa vitabu, kukuza lugha ya Kiswahili, kukuza utamaduni wa kusoma na kujisomea, pamoja na kuimarisha sekta ya uandishi na maktaba nchini.

Ameongeza kuwa idadi ya waandishi wanaoshiriki imeongezeka kwa kasi, huku washiriki wakitoka ndani ya nchi na Watanzania waishio nje ya nchi. Amebainisha kuwa uwiano wa ushiriki wa wanawake umefikia asilimia 33.3, jambo linaloonesha mwitikio chanya wa wanawake katika uandishi bunifu.

Kuhusu zawadi, Prof. Mlama amesema washindi wa nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu hupata zawadi mbalimbali, ambapo mshindi wa kwanza hunufaika kwa kuchapishiwa vitabu vyake na Serikali kununua na kuvisambaza katika shule za umma.

Aidha, Prof. Mlama amewakaribisha Watanzania wote kushiriki katika hafla rasmi ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025/2026, itakayofanyika Aprili 13 mwaka huu.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.