Na Mwandishi Wetu,
Tanga.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), akibainisha kuwa mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha ajira kwa Watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia manunuzi ya ndani yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 740 (sawa na takribani shilingi trilioni 1.9).
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika eneo la Chongoleani, mkoani Tanga, Dkt. Nchemba amesema mradi huo umefikia utekelezaji wa asilimia 81 na umeajiri Watanzania wapatao 8,500 sawa na asilimia 78 ya wafanyakazi wote 11,155.
“Mradi wa EACOP si tu ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, bali pia ni mshirika mkubwa wa maendeleo kwa kutoa fursa za ajira kwa wazawa, kuwajengea uwezo Watanzania na kuhusisha wakandarasi wa ndani,” alisema Dkt. Nchemba.
Ameongeza kuwa Serikali inajivunia mafanikio yaliyopatikana na dhamira ya wabia kuhakikisha mradi unakamilika katikati ya mwaka huu ili kuanza rasmi kusafirisha mafuta ghafi kwenda soko la kimataifa. Aidha, amesema utekelezaji wa mradi huo ni kielelezo cha ushirikiano imara kati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Nishati, Bi. Salome Makamba, amesema Serikali inayomiliki hisa asilimia 15 kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imeridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa. Amesema zaidi ya Watanzania 9,000 wameguswa na utekelezaji wa mradi huo na kulipwa fidia, wakiwemo wananchi 1,688 wa Mkoa wa Tanga waliolipwa shilingi bilioni 10.49, huku wengine wakipatiwa nyumba mbadala na msaada wa chakula kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja.
Ameongeza kuwa maelfu ya Watanzania wamefaidika na mafunzo ya bure kupitia vyuo vya ufundi stadi (VETA) pamoja na udhamini wa masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia ushirikiano wa mradi huo na taasisi hizo.
Kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), mradi huo umefadhili miradi ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 4.4, ujenzi wa Kituo cha Afya Donge mkoani Tanga na usambazaji wa umeme katika vijiji vilivyopitiwa na bomba katika mikoa nane, ambapo TANESCO inatarajiwa kuongeza mapato yake kwa kiasi kikubwa. Aidha, Bandari ya Tanga imeendelea kunufaika kutokana na uwepo wa mradi huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bi. Batilda Buriani, amesema mradi huo umeacha alama kubwa mkoani humo kwa kutoa ajira, mafunzo ya ufundi na ujasiriamali kwa wananchi ili waweze kuajiriwa na kujiajiri.
Ziara hiyo ilihusisha viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Matarajio, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa TPDC, na ilipokelewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP, Bw. Emmanuel Blarez, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Guillaume Dulout.
Mhandisi Mussa Msafiri alitoa maelezo ya kiufundi akibainisha kuwa ujenzi wa matenki manne ya kuhifadhi mafuta yenye ujazo wa lita 500,000 kila moja umefikia asilimia 87, huku ujenzi wa ghati ya kupakia mafuta kwenye meli ukifikia asilimia 57. Ujenzi wa miundombinu mingine ikiwemo majenereta, mfumo wa umeme wa jua na vifaa vya kuzimia moto unaendelea.
Naye msimamizi wa maudhui ya ndani (Local Content) wa EACOP, Bi. Neema Kweka, amesema mradi huo umetumia zaidi ya masaa milioni 40 kutoa mafunzo kwa wazawa na kufanya manunuzi ya ndani yenye thamani ya dola milioni 740, hivyo kusaidia kukuza uchumi wa ndani.
Bomba la EACOP lenye urefu wa kilometa 1,443 linaanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, na limepita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
Wanahisa wa mradi huo ni TotalEnergies (asilimia 62), TPDC (asilimia 15), Uganda National Oil Company (UNOC) (asilimia 15) na China National Offshore Oil Corporation (CNOOC) (asilimia 8).






Hakuna maoni: