RITA YATOA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MIRATHI NA UTATUZI WA MIGOGORO KWA VIONGOZI WA SERIKALI NA WAZEE WA KIMILA


Na Mwandishi Wetu, 

Katavi.

Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umeendelea kutoa mafunzo kwa viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tawala, Maafisa Tarafa, viongozi wa vitongoji pamoja na Wazee wa Kimila kutoka mikoa sita, ili kuwajengea uwezo wa kusimamia vyema migogoro inayotokana na masuala ya mirathi, ndoa na talaka katika jamii.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamewakutanisha viongozi kutoka mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mbeya na Songwe, na kufanyika mkoani Katavi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria katika masuala ya wosia, mirathi, ndoa na talaka ili kupunguza migogoro ya kifamilia na kulinda haki za warithi halali.

“Viongozi wa ngazi za msingi wana nafasi ya kipekee katika kutoa elimu kwa jamii na kusimamia utekelezaji wa sheria katika maeneo yao ya kazi, jambo litakalopunguza migogoro katika jamii,” alisema Bw. Kanyusi.

Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, washiriki wamepata uelewa kuhusu taratibu za uandishi na uhifadhi wa wosia, usajili wa mirathi pamoja na wajibu wa viongozi wa kimila katika kuhakikisha mgawanyo wa mali unafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi.

Bw. Kanyusi aliwahimiza viongozi hao kutumia sheria na taratibu zilizowekwa sambamba na busara katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, akisisitiza kuwa wao wapo karibu zaidi na jamii.

Kwa upande wake, Afisa Msajili Msaidizi Mkuu wa RITA, Bi. Victoria Mushi, ambaye ni miongoni mwa wawezeshaji wa mafunzo hayo, alielezea faida za mwananchi kuandika wosia mapema na kuhifadhi nyaraka hizo kwa mujibu wa utaratibu rasmi.

“Tumeshuhudia jamii nyingi zikiingia katika migogoro mikubwa ya mirathi kutokana na ukosefu wa elimu ya kuandaa wosia. Kupitia mafunzo haya, tuna uhakika migogoro hiyo itapungua kwa kiasi kikubwa,” alisisitiza Bi. Mushi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Bi. Jamila Yusuph, aliipongeza RITA kwa kuandaa mafunzo hayo na kusisitiza umuhimu wa viongozi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za RITA kupitia mfumo wa eRITA, hususan usajili wa ndoa, talaka, wosia na udhamini wa mirathi.

 “Mafunzo haya yataongeza uwazi katika utoaji wa huduma na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kulinda haki za wananchi na kupunguza migogoro,” alisema Bi. Yusuph.

Kwa upande wa viongozi wa kimila, Bw. Nelson Majura alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutoa mwongozo sahihi kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kimila katika kusimamia masuala ya mirathi.

Mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa RITA wa kuendelea kutoa elimu kwa umma na viongozi wa ngazi mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha haki, uwazi na utawala bora vinazingatiwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.