ACT WAZALENDO WAZINDUA MNARA WA KUMBUKIZI WA WAATHIRIKA WA OKTOBA 29 KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam. 

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 08,2026, cha ACT Wazalendo kupitia Ngome yake ya Wanawake kimezindua rasmi mnara wa kumbukizi kwa heshima ya waliopoteza maisha kufuatia matukio ya vurugu ya Oktoba 29, 2025. Uzinduzi huo umeelezwa kuwa sehemu ya kuenzi maisha ya marehemu na kuonesha mshikamano kwa familia zilizoathirika.

Akizungumza Machi 3, 2026 wakati wa hafla hiyo, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, amesema mnara huo ni ishara ya kumbukumbu, haki na matumaini ya taifa linalotaka kujijenga upya kwa misingi ya ukweli na uwajibikaji. Amesisitiza kuwa kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, ni muhimu kuangazia pia maumivu na changamoto wanazopitia wanawake, hususan mama waliopoteza watoto wao katika matukio hayo.

“Siku ya Wanawake si sherehe pekee, bali ni muda wa kutafakari hali halisi ya wanawake katika jamii. Machozi ya mama ni deni la taifa, na yanahitaji kusikilizwa kwa haki na huruma,” amesema.

Ameongeza kuwa taifa haliwezi kupata uponyaji wa kweli bila kukabiliana na ukweli wa yaliyotokea na kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika wote. Kwa mujibu wake, maridhiano ya kudumu yanahitaji uwazi, uwajibikaji na hatua madhubuti za kisheria.

Katika hatua nyingine, Semu ametoa wito wa kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi iliyo nje ya Serikali ili kuchunguza kwa kina matukio ya Oktoba 29, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kurejesha imani ya wananchi, kuimarisha utawala wa sheria na kujenga mshikamano wa kitaifa.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.