Na Francisco Peter,
Dar es Salaam.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameshiriki mbio za marathoni zilizoandaliwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) katika kuadhimisha miaka 20 ya taasisi hiyo. Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Dkt. Gwajima amesema TWCC imekuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake wengi nchini, kuanzia biashara ndogo na za kati hadi kufikia uchumi mkubwa. Ameeleza kuwa kupitia chemba hiyo, wanawake wamepata fursa ya kujifunza, kuimarisha mitandao ya kibiashara na kufungua masoko ndani na nje ya nchi.
“TWCC imekuwa daraja muhimu la kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwaunganisha na taasisi mbalimbali pamoja na fursa za kifedha na kibiashara,” amesema Dkt. Gwajima.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na TWCC ili kuhakikisha wanawake wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo na kuzitumia ipasavyo. Pia amewahimiza wanawake kuwa mstari wa mbele kulinda maadili ya jamii na kukataa vitendo vinavyoweza kusababisha mmomonyoko wa maadili.
Aidha, imeelezwa kuwa maelfu ya wanawake wamenufaika kupitia TWCC kwa kusajiliwa, kuimarisha biashara zao na kuongeza kipato, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa pato la taifa.
Katika maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na mbio za marathoni, Waziri Gwajima alikabidhi zawadi mbalimbali kwa washiriki, zikiwemo medali, kama ishara ya kutambua juhudi zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dkt. Mwajuma Hamza, amewashukuru wadhamini na washiriki wote kwa kufanikisha maadhimisho hayo, akibainisha kuwa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni kipaumbele muhimu katika safari ya maendeleo ya taifa.Imeelezwa kuwa mbio hizo hazikuwa tu mashindano ya riadha, bali ni ishara ya dhamira ya dhati ya kuendeleza ushiriki wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo, hususan katika kukuza biashara na uchumi wa nchi.


Hakuna maoni: