WADAU WA SOKO LA MITAJI WASIFU MWENDO WA SOKO NCHINI,MKURUGENZI WA CSD ASEMA HALI YA UWEKEZAJI IMEONGEZEKA


Wadau wa soko la mitaji wamekutana kujadili mustakabali wa maendeleo ya soko la hisa nchini, huku kongamano la uwekezaji ukilenga kuongeza uwazi, uwakilishi na ushiriki wa wawekezaji.

Akizungumza katika kongamano hilo Leo jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji wa CSD & Registry Company Limited, Benito Kyando, amesema lengo kuu la jukwaa ni kukutanisha wadau wa soko la mitaji ili kujadili mwelekeo wa soko, changamoto zinazokabili sekta na mikakati ya kuendeleza ukuaji wake.

Kyando amesema kampuni inaendelea kuimarisha mifumo ya usajili na utunzaji wa kumbukumbu za wawekezaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hatua inayolenga kurahisisha ushiriki wa wawekezaji mmoja mmoja na kuongeza ufanisi wa huduma.

Ameongeza kuwa mkutano huo umejikita pia katika utoaji wa elimu ya fedha kupitia semina mtandao (webinars), hasa kwa Watanzania waishio nje ya nchi, jambo lililochangia kuongezeka kwa ushiriki wa diaspora katika uwekezaji wa hisa.

Kwa mujibu wake, mwenendo wa soko unaonyesha ishara chanya baada ya thamani ya mauzo ya hisa kuongezeka kwa kasi ikilinganishwa na mwaka uliopita, hali inayoashiria kuimarika kwa uwekezaji na mwamko wa wananchi.

Aidha, amewahimiza wawekezaji kufuatilia kwa karibu uwekezaji wao na kusasisha taarifa zao mara kwa mara ili kuhakikisha wananufaika kikamilifu na fursa zilizopo, ikiwemo kupata gawio kwa wakati.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa elimu ya fedha, Edmund Munyagi, amesema mkutano kama huu ni chachu ya kuboresha ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji, akisisitiza umuhimu wa kuongeza elimu ya fedha na kuingiza somo hilo katika mitaala ya shule kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu.

Naye mdau wa soko la hisa, Emeliana Busara, amesema mkutano unatoa nafasi ya moja kwa moja kwa wawekezaji kupata taarifa sahihi na kuelewa mwelekeo wa soko, akibainisha kuwa ushiriki wa kidijitali na teknolojia unachangia kuimarisha imani na kuwahamasisha watu wengi kuwekeza.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.