Dar es Salaam
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Fedha (IFC) wamehimiza kuongezwa kwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ndani ya makampuni na taasisi mbalimbali nchini, wakieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukuza ustawi wa kibiashara.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Programu ya Wanawake na Uongozi, Mkuu wa Maendeleo ya Kibiashara wa DSE, Emmanuel Nyalali, amesema bado kiwango cha ushiriki wa wanawake katika uongozi ni cha chini, hali inayokwamisha ukuaji wa taasisi nyingi.
Nyalali amesema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa makampuni yanayowapa wanawake nafasi za uongozi hufanya vizuri zaidi kibiashara.
“Ni wazi kuwa taasisi zinazowajumuisha wanawake katika uongozi hupata mafanikio makubwa kutokana na sifa walizonazo, ikiwemo uaminifu, uwajibikaji na uwezo wa kujenga mahusiano mazuri kazini,” amesema Nyalali.
Ameongeza kuwa wanawake wana tabia ya kusikiliza na kujali ustawi wa wafanyakazi, jambo linalochochea ufanisi ndani ya taasisi, hivyo kutoa wito kwa makampuni yaliyosajiliwa DSE kuongeza uwakilishi wa wanawake katika ngazi za juu za uongozi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hazina wa Benki ya CRDB, Alex Ngusaru, amesema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi.
“Katika maandalizi ya utekelezaji wa programu hii kwa kushirikiana na IFC na DSE, sisi CRDB tayari tuna mifano hai; Mwenyekiti wa Bodi ni mwanamke, kiongozi wa foundation yetu ni mwanamke, na hata uongozi wa CRDB nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaongozwa na mwanamke,” amesema Ngusaru.
Ngusaru ameongeza kuwa ushahidi kutoka tafiti mbalimbali unaendelea kuthibitisha kuwa kampuni zinazoongozwa au kushirikisha wanawake katika uongozi hupata matokeo bora zaidi kiutendaji na kifedha.

Hakuna maoni: