MHANDISI MATIVILA AKAGUA MIRADI YA DMDP II, ATOA WITO UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU

Dar es Salaam.

‎Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema Serikali kupitia TARURA inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu mkoa wa Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wake ili idumu kwa muda mrefu.‎

‎Ameyasema hayo ‎wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa DMDP II katika Manispaa za Ubungo na Kinondoni, akisisitiza umuhimu wa kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati ili kuboresha miundombinu na maisha ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam.

‎Mhandisi Mativila alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya Msumi Km 9.9 na daraja la Msumi na ujenzi wa barabara ya Goba Wakorea km 7.76 zilizopo Ubungo pamoja na ujenzi wa barabara ya Mivumoni Km 4.79 iliyopo Kinondoni ambapo utekelezaji wa miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali.

‎Alibainisha kuwa kupitia mradi wa DMDP II, Manispaa ya Ubungo itanufaika na barabara za lami zaidi ya Kilomita 50, Manispaa ya Kinondoni zaidi ya Kilomita 40, huku mradi mzima wa DMDP II katika manispaa tano (5) ukifikia takribani Kilomita 250 za barabara, hatua inayotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii.

‎Aidha, ameonya kuhusu vitendo vinavyoweza kuhatarisha uendelevu wa miundombinu hiyo, hususani uchimbaji holela wa mchanga kwenye mito na utupaji wa taka hovyo kwenye mifereji, akisema vitendo hivyo vinaweza kusababisha uharibifu wa madaraja na barabara hata baada ya kukamilika na akisisitiza ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka za mitaa katika kulinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

‎Mhandisi Mativila pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema hatua hiyo imeanza kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za usafiri.

‎Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kutafuta rasilimali fedha ili kuboresha mtandao wa barabara za wilaya zinazosimamiwa na TARURA ili kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

‎Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Ubungo na Kinondoni wameishukuru serikali kwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwani itasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji na wananchi watazifikia huduma za kijamii na kiuchumi kwa haraka na urahisi.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.