ENG. ROSE MAYEMBE ANG’ARA KIMATAIFA KWENYE SEKTA YA MADINI


Kuelekea Kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.

KUTANA NA ENG. ROSE MAYEMBE: SAUTI YA TANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI KIMATAIFA

Katika juhudi za Tanzania kuendelea kung’ara kimataifa kupitia sekta ya madini, wanawake wa Kitanzania wameendelea kujipambanua katika majukwaa makubwa ya madini barani Afrika na duniani.

Hivi karibuni, katika Kongamano la African Mining Indaba lililofanyika nchini Afrika Kusini, Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wanawake Afrika (AWIMA) lilitoa tuzo kwa wanawake waliofanya vizuri katika sekta ya madini barani humo. Wanawake wawili kutoka Tanzania waliibuka washindi katika vipengele tofauti.

Miongoni mwao ni Mhandisi Rose Mayembe, ambaye alishika nafasi ya pili katika kipengele cha Leading Woman in Large-Scale Mining in Africa, akitanguliwa na mshindi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku mshindi wa tatu akitoka Afrika Kusini.


Eng. Rose Mayembe ni nani?

Akizungumza katika mahojiano maalum na Madini Diary, Eng. Rose Mayembe anasema yeye ni mhandisi na mtaalamu wa masuala ya mazingira na jamii katika sekta ya madini, akijikita katika uchimbaji endelevu na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Safari yake katika sekta ya madini ilianza takribani miaka 12 iliyopita aliposhiriki katika utekelezaji wa hatua za kufunga na baada ya kufunga mgodi mkubwa wa dhahabu wa Golden Pride Project (GPP) uliokuwa unamilikiwa na kampuni ya Resolute Mining wilayani Nzega, mkoani Tabora.

Anasema uzoefu huo ulimfundisha umuhimu wa kupanga mapema masuala ya mazingira na jamii katika miradi ya madini ili kupunguza athari kwa jamii na mazingira.

 “Hapo ndipo niliona umuhimu wa kuingiza fikra za mabadiliko ya tabianchi na ubunifu tangu mwanzo wa mradi,” anasema Rose.



Tuzo ya Mining Indaba na nyingine za kimataifa

Katika kongamano hilo la Mining Indaba, Rose alitambuliwa kama mshindi wa pili wa kipengele cha Leading Woman in Large-Scale Mining in Africa.

Anasema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwani jukwaa hilo hukutanisha serikali, wawekezaji, kampuni kubwa za madini pamoja na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Rose, ushindi huo unaonyesha uwezo wa wanawake wa Kitanzania kushindana na kuongoza katika sekta ya uchimbaji mkubwa.

 “Kwa wanawake, tuzo hii ni ishara ya kuvunja kizingiti cha glass ceiling na kuthibitisha kwamba tunaweza kuwa sehemu ya meza za maamuzi na kusukuma mbele ajenda ya madini yenye uwajibikaji na ushindani wa kimataifa,” anasema.

Mbali na tuzo hiyo, mwaka 2025 Rose alipokea pia Global Advocacy Award (GAA) katika kipengele cha Clean Energy & Sustainable Mining, wakati wa Global Advocacy Forum Awards (GAF 2025) zilizofanyika London, Uingereza.


Safari yake ya kazi

Kwa sasa, Rose anahusika katika miradi ya kitaifa na kimataifa akitoa mchango wake katika hatua zote za maisha ya mgodi, kuanzia usanifu wa migodi, uendeshaji, kufunga mgodi hadi hatua za baada ya kufungwa (post-closure).

Anasema lengo lake ni kuhakikisha sekta ya madini inaleta mapato kwa taifa huku ikilinda mazingira, kuheshimu haki za binadamu na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii.

“Nilipoanza kuzungumza kwa takwimu na maandalizi ya kitaalamu, niligundua kuwa uongozi si cheo bali ni uwezo wa kuathiri maamuzi. Tangu hapo sikuwahi tena kujiona kama mshiriki wa pembeni,” anasema.

Siri ya mafanikio yake

Rose anasema mafanikio yake yametokana na uamuzi wa ndani wa kujiamini na kutokusubiri kuthibitishwa na wengine katika sekta ambayo kwa muda mrefu imezoea kutawaliwa na sauti chache.

Anasisitiza kuwa kinachomtofautisha ni uwezo wa kuunganisha taaluma mbalimbali katika mtazamo mmoja wa kimkakati.

Kwa mujibu wake, sekta ya madini si uchimbaji pekee bali ni mfumo unaogusa uhandisi, mazingira, jamii, uchumi na sera.


Wanawake katika sekta ya madini

Eng. Rose anasema wanawake katika sekta ya madini — kuanzia wachimbaji hadi wataalamu — wanahitaji kuaminiwa na kupewa nafasi zaidi za uongozi.

 “Changamoto si uwezo, bali ni nafasi. Wanawake wanapaswa kushirikishwa katika maamuzi ya kimkakati, bodi na utungaji sera,” anasema.

Ushauri kwa wachimbaji wadogo

Akizungumzia sekta ya uchimbaji mdogo, Rose anashauri Serikali na wadau kuweka mkazo katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwarasimisha, kuwapatia mitaji, elimu ya biashara pamoja na mafunzo ya mazingira na usalama.

Anasema pia kuwepo kwa mwongozo rahisi wa tathmini ya athari za mazingira (EIA) na ufuatiliaji wa kitaalamu kutasaidia kuboresha sekta hiyo bila kuongeza mzigo wa kisheria.


Wito kwa wanawake na wasichana

Rose anatoa wito kwa wanawake na wasichana kujitokeza katika sekta ya madini, akisema sekta hiyo ni fursa ya ubunifu, taaluma na uongozi.

 “Jiwekezeni katika elimu na ujuzi. Uwezo hauna jinsia. Madini ni chachu ya maendeleo, lakini maendeleo ya kweli yanakuja pale wanawake na vijana wanaposhirikishwa kikamilifu,” anasema.

Anaongeza kuwa kizazi kijacho cha wanawake hakitahitaji kuomba nafasi, bali kitakuwa sehemu ya mwelekeo wa sekta ya madini.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.