FCC KUADHIMISHA SIKU YA HAKI YA MLAJI KWA KAMPENI KABAMBE YA ELIMU NCHI NZIMA


Na Mwandishi wetu,

Dar es Salaam. 

Tume ya Ushindani (FCC) imetangaza mpango maalum wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki ya Mlaji Duniani kwa kuendesha kampeni ya utoaji elimu itakayowahusisha walaji na wafanyabiashara kote nchini, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uelewa wa haki na wajibu katika soko.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, amesema maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuwawezesha walaji kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa au huduma, pamoja na kuwahamasisha kuchukua hatua wanapokutana na ukiukwaji wa sheria.

Amefafanua kuwa kampeni hiyo pia inalenga kuwajengea wafanyabiashara uelewa kuhusu wajibu wao wa kumlinda mlaji kwa kuzingatia matakwa ya sheria katika utoaji wa bidhaa na huduma, ili kujenga mazingira ya biashara yenye haki na uwazi.

Kwa mujibu wa FCC, kilele cha maadhimisho kitafanyika Machi 31, 2026 katika Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga.

Katika kufanikisha azma hiyo, Tume imeandaa ratiba ya vipindi maalum vya redio na televisheni pamoja na matumizi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Aidha, kliniki za walaji zitaendeshwa katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Musoma, Njombe na Tanga kwa lengo la kupokea na kushughulikia malalamiko, hoja na changamoto zinazowakabili walaji katika ununuzi wa bidhaa na huduma.

Sambamba na hilo, Machi 10, 2026 Tume itaendesha semina kwa wafanyabiashara na taasisi zinazotumia mikataba ya walaji (Standard Form Consumer Contracts) katika ofisi zake za Dar es Salaam, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uelewa kuhusu umuhimu wa mikataba inayozingatia haki za mlaji. Vilevile, Machi 11, 2026 kutafanyika semina maalum kwa wadau wa sekta ya ujenzi, wakiwemo wazalishaji wa nondo, bati, nyaya za umeme, rangi za majumbani pamoja na vyama vya kibiashara na wadhibiti wa kisekta.

Mbali na semina hizo, FCC pia itatumia magari ya matangazo (road shows) kufikisha elimu moja kwa moja kwa wananchi katika maeneo yao, ili kuongeza ushiriki na uelewa mpana wa masuala ya haki za mlaji.

Khadija Ngasongwa amewahimiza wananchi wenye changamoto zinazohusiana na bidhaa au huduma kufuatilia vipindi vya elimu vitakavyorushwa, kuhudhuria kliniki za walaji na kutumia fursa hiyo kuwasilisha malalamiko yao ili yapatiwe ufafanuzi na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.